Jan 20, 2024 13:49 UTC
  • Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran: Gaza imekuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani

Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika kikao cha Harakati ya Nchi Zisizofungamano ya Siasa za Upande Wowote (NAM) kinachofanyika Kampala nchini Uuganda kwamba: Mzingiro wa muda mrefu wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza umelifanya eneo hilo kuwa jela kubwa zaidi ya wazi duniani.

Mohammad Mokhber, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amehutubia kikao cha NAM mapema leo Jumamosi ambapo amegusia matukio ya Gaza na kusema hatua yoyote inayochukuliwa na Wapalestina ni haki yao ya asili. Amaeongeza kuwa: Juhudi za utawala wa Kizayuni wa Israel na washirikak wake wa Kimagharibi za kuyaarifisha mapambano halali ya ukombozi ya Wapalestina kuwa ugaidi hazina msingi wa kisheria na bali ni hila na udanganyifu.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza hatua ya kishujaa ya nchi ya Afrika Kusini ya kuwasilisha mashtaka dhidi ya utawala ghasibu wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu na kusema: Jinai za utawala wa Kizayuni za kuua watu zaidi ya 24,000 wasio na hatia, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, ni hadithi ya mauaji ya kimbari na ukatili uliopindukia unaofanywa dhidi ya taifa lenye utambulisho maalumu.

Huku akisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawataka wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote kutumia uwezo wao wa kisiasa na kiuchumi kukabiliana na utawala wa kibaguzi wa Israel, Mohammad Mokhber amesema kuwa, suala la kusitishwa vita mara moja huko Gaza, kufikishwa misaada ya kibinadamu katiikaa maeneo yote ya ukanda huo, kusitishwa kabisa sera ya kulazimisha watu kuhama wakazi yao na kuanza mara moja mchakato wa ujenzi mpya wa Gaza na maeneo mengine ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, vinapaswa kuwa katika ajenda na kupewa kipaumbele.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza pia kwamba, amani endelevu na ya kiadilifu huko Palestina inaweza kupatikana tu kwa kuhitimishwa uvamizi wa ardhi zote za Palestina, Syria na Lebanon, kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika nchi yao iliyoghusubiwa na kudhaminiwa haki ya kufanya maamuzi huru ya Wapalestina wote wa asili wanaoishi Palestina au walifukuzwa katika nchi yao kwa ajili ya mustakabali kupitia kura ya maoni ya umma.

Mohammad Mokhber pia amevitaja vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi kuwa ni mfano wa wazi wa ugaidi wa kiuchumi na kusema: Mataifa huru na yanayojitawala ya dunia hayakubali kutenzwa nguvu, kutwishwa matakwa ya wengine na kudhalilishwa, kwa sababu zama za kujichukua maamuzi ya upande mmoja na kuzitwisha nchi nyingine sera za siasa zako zimekwisha na kuyoyoma.

Tags