Kan'ani: Mashirika ya 'haki za binadamu' ya Magharibi hayana tena itibari
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mashirika yanayojidai kuwa ya kutetea haki za binadamu katika nchi za Magharibi yamepoteza itibari na uhalali wao kwa kufumbia macho jinai za kutisha zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Nasser Kan'ani amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter) na kuongeza kuwa, "Kuhusu mtihani wa Gaza, hakuna itibari iliyosalia katika taasisi na nara za kutetea haki za binadamu za nchi Magharibi. Barakoa katika uso bandia wa madai ya Magharibi ikiongozwa na Marekani ya kutetea haki za binadamu imeondolewa machoni pa walimwengu."
Amesema waungaji mkono wa jinai za kuogofya za utawala haramu wa Israel wanapaswa kuona haya kwa kuihadaa dunia kuwa ni watetezi wa haki za binadamu na wakati huo huo wanapuuza jinai za Wazayuni huko Gaza.
Kan'ani amekumbusha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umeua shahidi Wapalestina zaidi ya 26,000 wakiwemo watoto na wanawake 18,000 huko Gaza tokea Oktoba 7 mwaka uliopita, mbali na kufanya wakazi milioni 1.9 kati ya milioni 2.2 wa eneo hilo kuwa wakimbizi.
Amesema hatua ya Wamagharibi kuuunga mkono utawala wa Kizayuni kwa hali na mali inaonyesha unafiki, undumakuwili na uwongo wao wa wazi wa kudai kutetea haki za binadamu.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, hatua ya kisiasa ya baadhi ya nchi za Magharibi ya kudai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu na wakati huo huo kufumbia macho na kupuuza kabisa jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza ni fedheha kubwa.
Kan'ani amesisitiza kuwa, nchi hizo za Magharibi zenye historia ndefu ya ukiukaji wa haki za binadamu hazina ustahiki na hadhi ya kutoa nasaha kwa serikali na mataifa mengine duniani kuhusiana na masuala ya haki za binadamu.
Mapema leo asubuhi, maeneo ya kaskazini mwa Ukanda wa Gaza yamelengwa na kushambuliwa na ndege za kivita za utawala wa Kizayuni, ambapo Wapalestina wengine kadhaa wameuawa shahidi na wengine kujeruhiwa. Aidha wanajeshi wa utawala huo pandikizi wamevamia eneo la Qabatiya katika mji wa Jenin katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambapo wamekabiliwa na wanajihadi wa makundi ya muqawama.