Feb 01, 2024 07:15 UTC
  • Maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaanza rasmi nchini Iran

Alkhamisi ya leo ya tarehe Mosi Februari 2024 inasadifiana na tarehe 12 Bahman 1402 kwa kalenda ya Iran ya Hijria Shamsia. Tarehe kama hii kila mwaka huwa ndio mwanzo wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran.

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 12 Bahman 1357 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe Mosi Februari 1979, Imam Khomeini MA mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alirejea humu nchini baada ya kuweko uhamishoni kwa takriban miaka 15.

Kuwasili kwake humu nchini kuliharakisha kupatikana ushindi kamili wa Mapinduzi ya Kiislamu, siku kumi baadaye yaani tarehe 22 Bahman 1357 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 11 Februari 1979 Milaadia.

Ni kwa sababu hiyo ndio maana kuanzia siku kama ya leo ya tarehe Mosi Februari hadi tarehe 11 Februari, huwa ni kipindi cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran.

Hata mazingira ya hali ya hewa ya baridi kali na kunyesha theluji nyingi, hayawazuii wananchi wa Iran kujitokeza kwa wingi kwenye shehere za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Jana Jumatano, na ikiwa ni sehemu ya ufunguzi wa sherehe hizi kubwa za kitaifa humu nchini, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alizuru Haram ya Imam Khomeini MA kusini mwa jiji la Tehran na kumsomea Faatiha mwanachuoni huyo mkubwa wa zama hizi. 

Naye Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na baraza lake la mawaziri, walifanya ziara kwenye haram hiyo, jana Jumatano, na katika matamshi yake, Rais Raisi alisema, maisha yote ya Imam Khomeini yalikuwa ni ya kupinga uistikbari na kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran bado yako imara katika msimamo wake wa kupinga ubeberu Fikra hiyo imepata nguvu sana leo hii kote ulimwenguni kiasi kwamba katika kila kona ya dunia hivi sasa kunashuhudiwa hisia kali za kupinga uistikbari na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Tags