Iran yaitaka Marekani iache kutumia lugha ya vitisho dhidi yake
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameitaka Marekani iache kutumia lugha ya vitisho dhidi ya taifa hili na kusisitiza kuwa, vitisho vyovyote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu vitakabiliwa na jibu madhubuti na la haraka.
Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Mawaziri hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, muqawama katika eneo ni ukweli na uhalisia usiopingika mkabala wa uvamizi na vitisho.
Amesema Wamarekani wanajua vyema kwamba suluhisho la kumaliza vita na mauaji ya kimbari huko Gaza na mzozo wa sasa katika eneo la Asia Magharibi ni la kisiasa na kidiplomasia na sio vitisho na mabavu.
Indhari ya mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran imekuja baada ya Ikulu ya White House kuapa kwamba itatoa "jibu lenye athari kubwa" kwa shambulio la ndege zisizo na rubani lililolenga kambi ya Marekani kwenye mpaka wa Jordan na Syria.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kwamba, iwapo upande wowote utaishambulia ardhi ya Iran au maslahi yake na raia zake nje ya mipaka ya Iran, utakabiliwa na jibu madhubuti na kali.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) sambamba na kusisitiza kuwa, hakuna nchi yenye ujasiri wa kushambulia taifa na ardhi ya Iran amesema, "Hakuna kitisho chochote dhidi ya taifa hili kitakosa kupatiwa majibu."
Meja Jenerali Hossein Salami, Mkuu wa Jeshi la SEPAH amesema hayo baada ya Rais Joe Biden wa Marekani kuropoka kuwa Washington inaibebesha dhima Tehran kwa kushambuliwa kambi ya vikosi vamizi vya US katika eneo.
Iran imekanusha vikali kuhusika na shambulio la ndege zisizo na rubani lililolenga kambi ndogo ya Marekani nchini Jordan Jumapili ya Januari 28, ambapo wanajeshi 3 wa US waliuawa na wengine zaidi ya 40 walijeruhiwa.