Iran yalaani Magharibi kuisimamishia UNRWA misaada
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali hatua 'chungu' ya Wamagharibi ya kulisimamishia misaada Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Ijumaa, Nasser Kan'ani ameeleza kuwa, "Ni kinaya chungu kwamba nchi hizo (za Magharibi) zinaikatia misaada UNRWA kwa kutegemea madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na utawala ambao unatuhumiwa kufanya mauaji ya kimbari Gaza."
Kan'ani amebainisha kuwa, hakuna shaka kuwa hisia za kiutu zilizo na mwamko duniani zitahukumu uamuzi huo wa nchi za Magharibi wa kuwakatia misaada Wapalestina wakati huu ambao wanapitia mtihani na misukosuko.
Hivi karibuni, Ujerumani, Uswisi, Italia, Canada, Finland, Australia, Uingereza, Uholanzi, Marekani, Ufaransa, Austria na Japan zilitangaza kusitisha misaada yake kwa shirika la UNRWA kwa kutegemea madai ya Tel Aviv kwamba baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo wanaunga mkono oparesheni iliyotekelezwa na Harakati ya Hamas ya Kimbunga cha Al Aqsa mnamo Oktoba 7.
Nchi hizo za Magharibi zimesitisha misaada yao kwa Wapalestina katika hali ambayo, wakazi wa Ukanda wa Gaza wapatao milioni moja na laki tisa wamelazimika kuwa wakimbizi kufuatia jinai za miezi mitatu za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni katika eneo hilo.
Aidha asilimia 85 ya wakazi wa Gaza ambao wamekuwa wakimbizi wanakabiliwa na tatizo la dawa za matibabu, maji safi na chakula huku asilimia 60 ya miundomsingi ya ukanda huo ikiwa imeharibiwa kikamilifu.