Iran yazionya Marekani na Uingereza: Msijaribu kuzipima ghadhabu za mataifa ya eneo
(last modified Mon, 05 Feb 2024 06:46:53 GMT )
Feb 05, 2024 06:46 UTC
  • Iran yazionya Marekani na Uingereza: Msijaribu kuzipima ghadhabu za mataifa ya eneo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amelaani vitendo vya uchokozi vya hivi karibuni dhidi ya nchi za Asia Magharibi na kuzionya Marekani na Uingereza kwamba zisijaribu kuzipima ghadhabu za mataifa ya eneo hili.

Katika ujumbe alioandika kwenye akaunti yake ya X jana Jumapili, Amir-Abdollahian amesema Iran inalaani wimbi la hivi karibuni la mashambulizi ya anga ya Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen na mashambulizi mabaya ya majeshi vamizi na ghasibu ya Marekani dhidi ya maeneo kadhaa nchini Iraq na Syria.
 
Amesema, katika mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron, alimueleza kwamba "kuendelea kwa vita sio suluhisho," akimaanisha mazungumzo baina ya pande hizo mbili yaliyofanyika mwezi uliopita wa Januari kando ya mkutano wa 54 wa kila mwaka wa Jukwaa la Uchumi la Dunia mjini Davos, Uswisi.
 
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ametoa indhari kwa kusema: "Msijaribu kupima hasira za eneo. Tunauchukulia usalama wa Iraq, Syria, Yemen na Palestina (Gaza na Ukingo wa Magharibi) kuwa ni usalama wa eneo".

Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) ilisema katika taarifa siku ya Ijumaa kwamba vikosi vyake vilishambulia zaidi ya sehemu 85 "kwa ndege kadhaa" wakati wa uvamizi wa usiku ziliofanya katika maeneo ya Iraq na Syria.

Vyombo vya habari vya serikali ya Syria viliripoti kuwa uvamizi huo wa Marekani ulilenga maeneo kadhaa katika mkoa wa mashariki wa Dayr al-Zawr na mji wa Bukamal karibu na mpaka wa Iraq, lakini havikutoa maelezo kuhusu kiwango cha uharibifu na idadi kamili ya waliouawa.

Kwa mujibu wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq Muhammad Shia' al-Sudani, watu 16 waliuawa miongoni mwao wakiwamo raia na 25 walijeruhiwa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani nchini humo.

Katika hatua nyingine tena ya hujuma na uvamizi dhidi ya ardhi ya Yemen, Marekani na Uingereza usiku wa manane wa kuamkia jana zilifanya mashambulizi kadhaa ya anga kwenye mikoa ya Sana'a, Hudaydah na Sa'ada, mbali na mengine kadhaa.

Pentagon ilidai kuwa mashambulizi hayo yalilenga maeneo 13 ndani ya Yemen na kugonga vituo vya kuhifadhia silaha, mifumo ya makombora na ya urushiaji ambayo Vikosi vya Majeshi ya Yemen na harakati ya wananchi ya Ansarullah vinaitumia kushambulia meli za utawala wa Kizayuni wa Israel katika Bahari Nyekundu kuwaunga mkono Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.../

Tags