Feb 24, 2024 02:12 UTC
  • Biashara ya dola bilioni 55 ya Iran yafelisha vikwazo vya maadui

Thamani ya kiwango cha biashara baina ya Iran na nchi jirani imepindukia dola bilioni 55 ikiwa na maana kwamba, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani vimefeli na vimeshindwa kuizuia Jamhuri ya Kiislamu kufikia malengo yake.

Mohammad Rezvan Far, Mkuu wa Idara ya Forodha wa Iran amesema kuwa, kiwango cha mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na nchi jirani katika kipindi cha miezi 11 iliyopita kimeongezeka na kufikia dola bilioni 55 na milioni 275.

Mkuu huyo wa Idara ya Forodha ya Iran ameongeza kuwa, dola bilioni 25 na milioni 844 kati ya hizo ni za bidhaa za Iran zilizosafirishwa nje ya nchi na dola bilioni 29 na milioni 431 ni za bidhaa zilizoingia ndani ya nchi. 

Sehemu kubwa ya mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na nchi jirani imefanyika kati ya Tehran na nchi za Iraq, Uturuki, Jamhuri ya Azerbaijan, Turkmenistan, Armenia, Kuwait, Qatar, Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Nchi za Kiarabu (Imarati), Pakistan, Afghanistan, Oman, Russia, Kazakhstan na Bahrain. 

Uchumi wa Iran ni wa kimuqawama

 

Takwimu hizo zinaonesha mafanikio ya serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kutafuta masoko mapya licha ya kuwepo vikwazo vya Marekani na waitifaki wake wa Magharibi dhidi ya Iran.

Biashara ya Iran inayotegemea kusafirisha nje bidhaa za mashirika yenye msingi wa kielimu na teknolojia mpya imeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni kati ya Tehran na nchi jirani.

Wataalamu na wanasayansi vijana wa Iran kwa uungaji mkono wa serikali kupitia taasisi ambazo msingi wake ni elimu, wamekuwa wakifanya jitihada kubwa kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya maadui wanaoongozwa na Marekani na wamepata mafanikio makubwa katika jitihada zao hizo ambayo yanapongezwa na hata wataalamu wa nje ya Iran.

Mashirika ya Iran ambayo msingi wake ni elimu yanashiriki na kuonesha bidhaa katika viwango vya juu kimataifa na kushindana kiubora na bidhaa za mashirika maarufu duniani na tena basi bei ya bidhaa hizo za Iran ni nafuu ikilinganishwa na bidhaa kama hizo za nje ya nchi.

Kama katika miaka ya huko nyuma, bidhaa za Iran zilizokuwa zinasafirishwa nje ya nchi zilihusiana tu na mafuta, gesi na baadhi ya bidhaa maalumu, katika miaka ya hivi karibuni mashirika ya kielimu ya Iran yamefanya maajabu ya kuzalisha bidhaa za kila namna za viwango bora na kufikia hata kupongezwa na wataalamu wa nje ya nchi.

Sera bora za Iran zinaendelea kusambaratisha vikwazo vya maadui

 

Masoko ya bidhaa za Iran hayaishii tu kwa nchi jirani, bali nchi za bara la Afrika na Amerika ya Latini nazo zimepokea vizuri bidhaa za Iran. Ni kwa sababu hiyo ndio maana katika miaka ya hivi karibuni, Marekani na waitifaki wake wa Magharibi wamezidisha njama zao za kujaribu kufelisha bidhaa za Iran kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo za kuziwekea vikwazo bidhaa hizo. Lakini njama hizo zimefeli kutokana na umakini wa sera na siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya majirani zake.

Nafasi bora ya kijiografia ya Iran, vyanzo adhimu vya kimaumbile, uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa za kila namna za bei nzuri na ubora wa hali ya juu ni mionogni mwa sifa maalumu za bidhaa za Iran zinazosafirishwa nje ya nchi. 

Marekani na nchi zinazolifuata kibubusa dola hilo la kiistikbari katika vikwazo vyake dhidi ya Iran zinaelewa vyema kuwa, vikwazo vyao havina athari kwa Jamhuri ya Kiislamu kwani mazingira yalivyo leo duniani yenyewe yanafelisha vikwazo hivyo.

Daima Iran ya Kiislamu inaweka sera nzuri za kuwa na uhusiano mzuri wa kibiashara na nchi nyingine kwani inaamini kuwa uhusiano huo lazima uende sambamba na ustawi wa uhusiano wa kisiasa baina yake na nchi hizo kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi na kisiasa kwa wakati mmoja.