Feb 25, 2024 07:51 UTC
  • Ukuaji wa uchumi sambamba na kupungua mfumuko wa bei nchini Iran

Ripoti mpya ya Kituo cha Takwimu cha Iran inaonesha kuwa, ukuaji wa uchumi uliendelea kuimarika katika robo ya tatu ya mwaka huu licha ya kutekelezwa sera za kudhibiti mfumuko wa bei nchini.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Kituo cha Takwimu cha Iran, uchumi wa nchi uliendelea kukua katika robo ya tatu ya mwaka ambapo Pato Jumla la Taifa lilikuwa kwa asilimia 5.1 likijumuisha mafuta, na kwa asilimia 2.5 bila mafuta.

Pia, ukuaji wa Pato la Taifa katika miezi 9 ya kwanza ya mwaka huu wa Kiirani (1402) ikijumuisha sekta ya mafuta na gesi, ulikuwa wa asilimia 6.7 na ukiondoa sekta ya mafuta na gesi ulikuwa wa asilimia 4.2.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa licha ya kutekelezwa sera za kubana matumizi, lakini bado uchumi wa Iran uko kwenye njia ya ukuaji chanya. Hatua madhubuti ambazo zimechukuliwa katika muelekeo wa kutumia vizuri fedha za taifa sambamba na kuunga mkono uzalishaji wa ndani, ni kiashiria cha kustawi uchumi wa nchi katika fremu ya kauli mbiu ya mwaka ambayo ni kuunga mkono ukuaji wa uchumi na kupunguza mfumuko wa bei. Kwa hakika, ukuaji uchumi katika kipindi cha miaka 2 ya serikali ya 13 ikilinganishwa na miaka ya nyuma, unaonyesha wazi mabadiliko makubwa ambayo yamefanyika katika uwanja wa uchumi na uzalishaji bidhaa na wakati huo huo kupungua kwa mfumuko wa bei ndani ya nchi.

Farshad Moghimi, Naibu Waziri wa Usalama na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwanda Vidogo na Maeneo ya Viwanda nchini anasema kuhusu suala hilo: 'Tangu mwanzoni mwa mwaka 1402 hadi sasa, kupitia ufufuaji wa vitengo vya uzalishaji vilivyosimama, kufunguliwa miradi mipya na kuongeza uwezo wa viwanda kuzalisha bidhaa katika maeneo ya viwandani kumeibua ajira mpya elfu 64, 134 katika maeneo hayo.'

Katika upande mwingine, kufikiwa ukuaji wa asilimia 6.7 ya uchumi wa Iran katika kipindi cha miezi 9 ya mwaka huu (1402) kumetimia baada ya Benki Kuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutekeleza sera mbalimbali za kupunguza mfumuko wa bei.

Nyingi ya sera hizo kwa kawaida huwa na taathira hasi katika ukuaji wa uchumi, lakini pamoja na hayo tunaona kwamba utekelezaji wa sera mbalimbali za kusaidia shughuli za uzalishaji na uchumi, umeimarisha uchumi na wakati huo huo kupunguza mfumuko wa bei nchini.

Kupunguzwa ushuru wa vitengo vya uzalishaji kutoka asilimia 25 hadi asilimia 18, kurahisishwa utolewaji leseni za biashara, kutekelezwa sera mbalimbali kwa ajili ya kudhamini mahitaji ya vitengo vya uzalishaji, kubadilishwa muundo wa gharama za bajeti ili kuongeza bajeti ya ujenzi na miundombinu, ni baadhi ya mambo ambayo yamechangia ukuaji wa uchumi wa nchi, licha ya kutekelezwa sera za kupambana na mfumuko wa bei.

Ukuaji wa uchumi ni moja ya viashiria muhimu na vya kawaida ambavyo hutumika kutathmini muelekeo wa uchumi katika nchi nyingi duniani, na ikiwa ukuaji wa juu wa uchumi utaendelea, bila shaka utaleta maendeleo makubwa nchini.

Hivi karibuni Benki ya Dunia ilithibitisha katika ripoti yake kuhusu viashiria vya uchumi wa Iran na kusema kwamba serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa katika "kuleta utulivu katika soko la fedha za kigeni" na "kudhibiti matokeo ya mfumuko wa bei".

Katika ripoti yake ya karibuni kuhusu hali ya uchumi wa dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa IMF limetangaza kuwa, ukuaji wa uchumi wa Iran mwaka 2023 ulikuwa wa asilimia 5.4. Ukuaji huo wa kutia moyo ulikuwa haujawahi kushuhudiwa tena katika miaka ya hivi karibuni, na ndio ukuaji mzuri zaidi tangu Marekani ilipojiondoa katika mapatano ya JCPOA mwaka 2018 na kuanza kutekeleza siasa za mashinikizo ya juu zaidi ya kisiasa na kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa mujibu wa IMF, Iran ilikuwa na ukuaji wa juu zaidi wa uchumi mwaka 2023 kati ya nchi 30 za juu za uchumi duniani baada ya India. Nchi hizo 30, ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 83 ya uchumi wa dunia, zinajumuisha nchi zilizoendelea kiviwanda kama vile Marekani na Ujerumani na nchi zinazoendelea kama vile Iran, Uturuki, Korea Kusini na China.

Kwa hiyo, maamuzi ya serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu katika kubadilisha vipaumbele na malengo ya kiuchumi yamekuwa na matokeo chanya na ya kuridhisha katika kutatua changamoto muhimu za kiuchumi nchini. Dawood Mandhur, mkuu wa Shirika la Mipango na Bajeti nchini, aliandika hivi mwezi uliopita akiashiria ripoti ya Kituo cha Takwimu cha Iran kuhusu kupungua kwa kiwango cha mfumuko wa bei nchini: 'Ujumuishwaji makini wa sera za pesa na fedha za kigeni za serikali unatoa matumaini ya kuondolewa mdororo wa uchumi na kudhibitiwa mfumuko wa bei nchini. Ukuaji wa uchumi usio na mfumuko wa bei bila shaka unajitajia ushirikiano wa idara zote za serikali, umma na binafsi.'