Marekani itajuta ikikiuka mapatano ya nyuklia ya Iran
Afisa wa ngazi za juu nchini Iran ameionya vikali Marekani kuwa itajuta iwapo itakiuka mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.
Ali Akbar Salehi Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu inafungamana kikamilifu na utekelezwaji wa mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA yaliyofikiwa Julai 2015 baina ya Iran na kundi la 5+1.
Salehi aidha amesema kuwa utekelezwaji wa JCPOA utakuwa kwa maslahi ya Iran, nchi za Magharibi, Mashariki ya Kati na dunia nzima kwa ujumla. Hata hivyo ameonya kuwa, ukiukwaji wa mapatano hayo utakuwa kwa hasara ya kila mtu.
Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilianza kutekeleza JCPOA Januari 16.
Chini ya mapatano hayo, Iran inaondolewa vikwazo vya kinyuklia vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya, Baraza la Usalama na Marekani mkabala wa kupunguza baadhi ya shughuli zake za nyuklia.
Hata hivyo benki za Ulaya zinajizuia kufanya biashara na Iran kwa kuhofia kuadhibiwa na Marekani.
Juni 14 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema Marekani haijatekeleza kiwango kikubwa cha ahadi zake katika mapatano ya JCPOA na kwamba Iran imetekeleza ahadi zake. Kiongozi Muadhamu aliashiria matamshi ya baadhi ya wagombea urais Marekani waliosema watayachana mapatano ya nyuklia na kusema wakifnaya hivyo Iran itauchoma mkataba huo.