Venezuela yaipongeza Iran kwa kufanikisha uchaguzi
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uchaguzi uliofanikiwa. Katika ujumbe wa pongezi uliotumwa kwenye mtandao wa X, zamani wa Twitter, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Yvan Gil, alisifu ustaarabu na shauku ya watu wa Iran waliohudhuria uchaguzi huo.
Afisa huyo wa Venezuela amewapongeza wananchi na serikali ya Iran kwa zoezi lao la kidemokrasia katika uchaguzi wa Ijumaa wa kuchagua wawakilishi wa wananchi katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge), pamoja na Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu.
Gil, ambaye alikuwa akiwasilisha salamu za pongezi kwa niaba ya Maduro na serikali ya Venezuela, amewasifu watu wenye busara wa Iran waliohudhuria uchaguzi huo ili kuzuia njama zisizoisha za adui dhidi ya umoja wao.
Matokeo ya awali ya uchaguzi wa Bunge la Iran na Baraza la Wataalamu yameonyesha Jumamosi kuwa zaidi ya asilimia 40 ya wapiga kura waliotimiza masharti walishiriki katika uchaguzi huo.
Gil alisema uwepo mkubwa wa umma katika uchaguzi huo ulihalalisha uchaguzi na ni ishara ya dhamiri ya wapiga kura, na ari kwa nchi yao, akibainisha kuwa uchaguzi wa Iran ulikuwa "nembo ya wazi ya mshikamano na umoja wa kitaifa katika taifa la Uajemi."
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran imesema kati ya jumla ya watu milioni 61.17, wakiwemo wanaume milioni 30.94 na wanawake milioni 30.22 waliostahili kupiga kura katika chaguzi hizo mbili, zaidi ya watu milioni 25 walipiga kura kuwachagua wabunge 290, na wajumbe 88 wa Baraza la Wataalamu.
Rais Ebrahim Raeisi wa Iran amesema kuwa, kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo, taifa la Iran kwa mara nyingine limezuia njama za maadui wa nchi hiyo na kudhihirisha muono na busara zao na kuijaza fahari Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.