Mar 26, 2024 07:49 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akosoa undumakuwili wa Magharibi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumza kwa simu na mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya katika Masuala ya Nje na Sera ya Usalama na kukosoa vikali vigezo vya undumakuwili na vinavyokinzana vya nchi za Magharibi mkabala wa Palestina na Gaza.

Hossein Amir-Abdollahian amezungumza kwa simu na Josep Borrell ambapo wamechunguza na kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya karibuni muhimu kikanda na kimataifa na uhusiano kati ya Iran na Umoja wa Ulaya. Abdollahian amesema kuwa kuendeleza mgogoro wa kibinadamu na hatua ya utawala wa Israel ya kuwasababishia njaa wakazi wa Ukanda wa Gaza vimeifanya hali ya mambo ya eneo hilo kuwa "mgogoro halisi wa karne." 

Amir Abdollahian ameashiria hali ya sasa huko Ukanda wa Gaza na kutolewa ripoti za kutisha kuhusu kunyongwa Wapalestina katika hospitali ya al Shifa na kuuliwa kwa umati wanawake na watoto na jeshi ghasibu la Kizayuni na kuongeza kuwa: Kwa bahati mbaya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni analiichukulia faili la Gaza na hata maslahi ya taifa ya Marekani kama mateka wa maslahi yake binafsi.  

Mashambulizi ya kikatili ya Israel nje ya hospitali ya al Shifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepongeza mtazamo wa Borrell kuhusu ulazima wa kusimamishwa vita na kutumwa misaada ya haraka ya kibinadamu huko Gaza na kukumbusha wajibu wa jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Ulaya katika kadhia ya Palestina.

Amesema, wakati umefika wa kuchukuliwa hatua za kuuadhibu utawala wa Israel; na kuundwa kundi la kimataifa kwa ajili ya kuchunguza jinai za utawala huo zikiwemo zile zilizofanywa katika hospitali ya Al Shifa. 

Tags