Sisitizo la Pakistna la kuhitajia mno gesi ya Iran
(last modified Sat, 30 Mar 2024 02:31:49 GMT )
Mar 30, 2024 02:31 UTC
  • Sisitizo la Pakistna la kuhitajia mno gesi ya Iran

Musadik Masood Malik, Waziri wa Mafuta wa Pakistan amesema kuwa nchi yake inahitajia mno gesi ya Iran na kwamba msimamo wa Islamabad uko wazi kuwa, kukamilishwa mradi wa kupelekwa gesi ya Iran nchini Pakistan ni jambo la dharura.

Waziri huyo wa mafuta wa Pakistan amedai pia kwamba nchi yake infanya juhudi za kweli za kuhakikisha mradi wa bomba la gesi ya Iran kuelekea nchini mwake unakamilishwa.

Ijapokuwa serikali mpya ya Pakistan inazungumzia suala la kustawishwa uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na imeahidi kuwa itahakikisha mradi wa bomba la gesi ya Iran kuelekea nchini Pakistan unafanikishwa, lakini kuna wajibu wa kufanyiwa tathmini na kuchunguzwa ukweli wa madai hayo. Hii ni kwa sababu hivi sasa ni takriban miongo mitano imepita lakini serikali zote zilizoingia madarakani huko Pakistan zimeshindwa kutekeleza ahadi zao kuhusu mradi huo.

Mohsen Ruyi Sefat, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Ni karibu miongo mitano imepita sasa tangu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipokuja na wazo la kuiuzia Pakistan gesi na kujenga bomba la gesi kuelekea Bara Hindi kwa jina la Bomba la Amani. Lakini licha ya ahadi zinazotolewa na tawala zinazoingia na kutoka madarakani huko Pakistan, lakini hakuna serikali hata moja ya nchi hiyo iliyoheshimu ahadi zake na hadi hivi sasa mradi wa bomba hilo haujakamilika."

Iran imetekeleza wajibu wake wa kulifikisha bomba la gesi hadi kwenye mpaka wa Pakistan lililobakia ni viongozi wa Islamabad kuingiza gesi hiyo nchini mwao.

 

Katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza vizuri ahadi zake kuhusu mradi huo kiasi kwamba imeshalifikisha bomba hilo hadi kwenye mpaka wa Pakistan. Lakini kutokana na mirengo ya kisiasa na kijeshi inayotawala huko Pakistan, nchi hiyo imeshindwa kuendeleza na kukamilisha sehemu iliyosalia ya mradi huo. Mashinikizo ya Marekani ambayo haitaki mradi huo ukamilike, kwa upande fulani yamezizuia tawala zinazoingia madarakani nchini Pakistan kuchukua hatua za kweli za kuufanikisha mradi huo muhimu ambao viongozi wote wa Pakistan wanasema kuwa ni mradi wa dharura kwa nchi yao.

Ni kutokana na kukiri udharura huo ndio maana viongozi wa Pakistan akiwemo waziri wa mafuta wa nchi hiyo, sasa wamejitokeza wazi zaidi kuilaumu Marekani kwa kukwamisha mradi huo licha ya kujua vyema kwamba ni muhimu sana kwa Pakistan. Kinachoonekana kuwakasirisha zaidi viongozi wa Pakistan angalau kidhahiri ni kuona kuwa nchi zinazopakana na Iran zinanufaika vizuri na fursa zinazotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zikiwemo nchi za Iraq na Uturuki na wanashangaa kwa nini nchi yao ya Pakistan inapoteza fursa hizo kwa mashinikizo ya Marekani. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikwamishwi na mashinikizo hayo ya Marekani na imetekeleza vilivyo ahadi zake za kulifikisha bomba hilo la gesi hadi kwenye mpaka wa Pakistan, hivyo ni viongozi wa Islamabad ndio wanaopaswa kuchukua msimamo imara wa kutokubali kuburuzwa na mashinikizo ya Marekani.

Kiujumla ni kwamba hivi sasa Tehran inaisubiri Pakistan itekeleze majukumu yake katika suala hilo. Karibu mwezi mmoja nyuma, waziri wa mafuta wa Pakistan alitoa tamko na kusema kuwa kukamilishwa mradi wa bomba la gesi ya Iran kutaifanya nchi yake kuwa na usalama wa nishati na kufaidika sana katika kudhamini mahitaji yake makubwa. Aliafiki kuanza kutengenezwa bomba la kilomita 81 kutoka ndani ya Pakistan hadi kwemye mpaka wa nchi hiyo na Iran. Lakini lililo muhumu ni kuona ahadi hizo zinatekelezwa kivitendo, si maneno matupu. Hasa kwa kuzingatia kuwa viongozi na wataalamu wote wa masuala ya kiuchumi wanasema kuwa Pakistan haina chaguo jingine ila kufaidika na utajiri wa nishati wa Iran kama inataka kweli kupambana na mgogoro wake mkubwa wa nishati na kuwadhaminia Wapakistan nishati ya uhakika na ya gharama nafuu.