Apr 21, 2024 02:19 UTC
  • Iran yaitoza Marekani faini ya dola bilioni moja kwa kuunga mkono jinai za utawala wa Kipahlavi

Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeitoza Marekani faini ya dola bilioni moja kwa kuunga mkono jinai za utawala wa Kipahlavi uliokuwa madarakani Iran kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika Rasmi la Habari la Iran (IRNA), hukumu hiyo imetolewa katika kesi iliyowasilishwa mbele ya Tawi la 55 la Mahakama ya Umma Tehran inayoshughulikia kesi za kimataifa. 

Kesi hiyo ilifikishwa mbele ya mahakama na watu 15 ambalo walikuwa wafungwa wa kisiasa Iran kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Serikali ya Marekani imehukumiwa faini ya dola bilioni moja kutokana na kushiriki katika kuundwa SAVAK (Idara ya Kijasusi na Usalama wa Taifa Iran wakati wa utawala wa kifalme wa Pahlavi), na halikadhalika kutokana na uungaji mkono wake utawala wa kidikteta wa Pahlavi. Fedha hizo zinalenga kuwalipa fidia kwa walioteswa na shirika hilo la SAVAK.

Nyaraka zilizowasilishwa Mahakamani zinaonyesha kuwa, serikali ya Marekani, ikiwa inafahamu kikamilifu kuhusu jinai za kinyama za utawala wa kidikteta wa Pahlavi dhidi ya wananchi Iran, iliwasilisha mpango wa kuunda SAVAK kwa utawala wa Pahlavi. Baadaye maafisa wa serikali ya Marekani walitoa msaada na mafunzo kwa makachero wa SAVAK ambao walihusika katika kuwakamata, kuwatesa na hata kuwaua wafungwa wa kisiasa nchini Iran.

Mahakama imefahamishwa kuwa, mbali na kusaidia kuunda shirika  katili la SAVAK, Marekani pia ilikiuka  kanuni za kibinadamu kwa kuunga mkono jinai za shirika  hilo la utawala wa kiimla wa Pahlavi.

Mahakama imesema faini hiyo ya dola bilioni moja itatumika kugharamia  matibabu, na kufidia madhara yatokanayo na majeraha ya mwili,  maumivu na mateso na masaibu yaliyosababishwa na magonjwa yatokanayo na mateso makali na kuwekwa kizuizini.

 

 

Tags