Apr 25, 2024 07:32 UTC
  • Ebrahim Raisi: Iran na Sri Lanka zimeazimia  kuimarisha ushirikiano baina yao

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, hakuna kikwazo chochote katika kustawisha uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Sri Lanka.

Ebrahim Raisi amesema hayo akiwa safarini nchini Sri Lanka na kueleza bayana kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na serikali ya Sri Lanka zimeazimia kuendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano baina yao katika nyanja zote na katika ngazi zote na kwamba, jambo hilo ni kwa maslahi ya mataifa hayo mawili. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Sri Jayawardenepura Kotte akkiwa na mwenyeji wake Rais Ranil Wickremesinghe amesema, uhusiano kati ya Iran na Sri Lanka hususan baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu umeingia katika hatua mpya na unaendelea kustawi. Aidha amesema, katika mazungumzo yaliyofanyika baina ya viongozi wa ngazi za juu wa nchi hizo mbili, kumetiliwa mkazo juu ya suala la kuongezwa kiwango cha ushirikiano baina ya pande mbili katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kibiashara, kiutamaduni, utalii, sayansi na teknolojia.

Dkt. Raisi amebainisha utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuipatia Sri Lanka uzoefu wa huduma za kiufundi na kiuhandisi kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa nchhi hiyo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais wa Iran amezungumzia suala la Palestina kuwa suala muhimu zaidi duniani daghadagha na hangaiko kuu la mataifa yote na kusema: Kinachotokea leo, jinai zinazoendelea na za kutisha huko Gaza, zimezua wasiwasi mkubwa na mshangao kwa watu wote wa dunia, na swali lao ni kwa nini mashirika ya Kimataifa na haki za binadamu hayatekelezi wajibu wao katika uwanja huu?

 

Dakta Raisi sambamba na kueleza kuwa, mauaji ya watoto na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Gaza yamehuzunisha na kuathiri sio tu Umma wa Kiislamu bali pia wafuasi wa dini nyingine duniani amefafanua kwa kusema kuwa, kinachosikitisha zaidi ni kwa nini na kwa mantiki ipi jinai na uhalifu huu unaungwa mkono na Marekani na mataifa mengine ya Magharibi? Na kwa nini Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama zimefubaa na kutokuwa na utendaji na hazichukui hatua madhubuti kuzuia uhalifu huu?