"Mauaji ya watoto 15,000 wa Gaza yanaashiria mwisho wa Israel"
(last modified Wed, 15 May 2024 03:19:13 GMT )
May 15, 2024 03:19 UTC

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hakuna shaka kuwa mauaji ya watoto zaidi ya 15,000 wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza itakuwa chachu ya kuharakisha mchakato wa kuporomoka na kusambaratika utawala wa Kizayuni wa Israel.

Rais Ebrahim Raisi aliyasema hayo jana Jumanne akihutubia Kongamano la 5 la Imam Ridha (AS) katika mji wa Mashhad wa kaskazini mashariki mwa Iran na kuongeza kuwa, jinai za Israel zimeifanya dunia iwe na hamu ya kuwepo nidhamu mpya yenye uadilifu.

Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, "Hatuna shaka kuwa, damu zilizomwagwa ardhini za watoto 15,000 wa Kipalestina, zitahitimisha maisha ya Wazayuni, na kuifanya nidhamu ya sasa ya dunia kuwa ya kiadilifu."

Amesisitiza kuwa: Jamii ya mwanadamu hii leo imegundua kuwa, utawala wa Kizayuni ni saratani ambayo inapasa kumalizwa, ili eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na dunia kwa ujumla zipate amani na usalama. 

Maiti za watoto wa Gaza

Rais wa Iran amepongeza mapambano ya miezi saba wa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza dhidi ya adui Mzayuni na kusisitiza kuwa, licha ya jinai zisizo na kifani zinazofanyika Gaza, lakini wananchi wa eneo hilo wanaendelea kupata ushindi katika medani ya vita, na hakuna shaka hatimaye adui Mzayuni atashindwa.

"Damu za watoto wa Gaza zitalipiza kisasi dhidi ya Mafarao wa enzi hizi, kama ilivyoshuhudiwa katika kisa cha Firauni na Nabii Musa AS," ameongeza Sayyid Raisi.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria maandamano ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Mashariki na Magharibi wakitaka kuhitimishwa dhulma za Uzayuni na kukombolewa Palestina na kueleza kuwa: Ulimwengu leo hii umeelewa kuwa, mfumo unaotawala hivi sasa duniani si wa kiadilifu, na unapasa kubadilishwa.

Tags