May 27, 2024 08:14 UTC
  • Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu: Bunge linapaswa kuleta utulivu na matumaini

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kuanza kazi Awamu ya 12 ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge), amesisitiza kuhusu kuwepo Bunge lenye uwiano, mwingiliano wenye nidhamu na mshikamano na mihimili mingine ya dola na pia ndani yake liwe lenye usahihi na subira.

Aidha amesisitiza kuwa bunge linapaswa kuwa lenye kuleta matumaini kila wakati na lihimize jitihada za maelewano na udugu katika mazingira ya umma nchini.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake Jumatatu asubuhi kwa mnasaba wa ufunguzi wa Awamu ya 12 ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu,  amesema kuzivutia nyoyo za wananchi na kutenda mema ni mambo ambayo yatakuwa na malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa:  Kushiriki mamilioni ya wananchi katika mazishi ya shahidi Rais Sayyid  Ebrahim Raisi na mashahidi wenzake ni mfano wa malipo haya kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: "Hivi sasa awamu ya 12 ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu inaanza kama kawaida katika tarehe iliyopangwa na bila kuchelewa, nanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu mpendwa na mwenye hekima na kushukuru kutokana na kuendelea na kuimarika kwa demokrasia ya kidini, ambayo ni zawadi kubwa kwa taifa la Iran."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kila bunge jipya linaweza kutengeneza mwangaza mpya katika upeo angavu wa nchi na kuongeza matumaini na hamasa ya taifa kwa kutumia mamlaka yake katika sheria. Amesema bunge hilo litaweza kuchanganya usasa na uvumbuzi, ukomavu na umakini na kuweka sheria na kutekeleza majukumu ya usimamizi mbali na misukosuko na mikwaruzano.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, nukta ninayosisitiza daima ni kwamba Bunge linapaswa kuwa na utulivu, lenye kuleta matumaini, hamasa na kukaribisha hisia ya udugu katika mazingira ya umma nchini. Katika bunge lenyewe, mashindano yasiyo na maana kwenye vyombo vya habari na mabishano yenye madhara kisiasa hayapaswi kuchukua muda mafupi uliopo wa kufanya kazi; vinginevyo, uwezo na thamani ya uwepo wa wawakilishi katika nafasi hii ya juu utapotea na hii ni hasara kubwa.

Ayatullah Khamenei amesema, nukta nyingine kuhusu kiapo cha wabunge ni kwamba kiapo hiki si maonyesho au urasimu tu; Ni kiapo cha kweli na cha kuwajibika ambacho kitakuwa cha uwajibikaji katika ulimwengu huu na ujao. Waheshimiwa wawakilishi lazima waweke kiapo hiki mbele ya macho yao wakati wote wa uwakilishi wao na kukizingatia kama kigezo cha kupima utendakazi wao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, nukta nyingine inahusiana na masuala ya lazima na kimaadili, mtindo wa maisha ya Kiislamu ambao ni sehemu muhimu ya maadili mema ambayo ni muhimu sana katika uga wa changamoto za kisiasa na mashindano halali. Ni hapa ndipo ucha Mungu na kusameheana, haki, uaminifu, wajibu na kazi isiyo na ubinafsi huonyesha thamani yake kuu. Mashahidi wa  helikopta - (Mashahidi Seyed Ebrahim Raisi na timu iliyoandamana naye), ambao sasa wanaombolezwa na nchi nzima - moja ya sifa zao ilikuwa kuzingatia maadili mema. Kujichunga katika uwanja huu kunapaswa kuchukuliwa kwa uzito.

Ayatullah Khamenei amesema, nukta ya mwisho ni kukumbuka ukweli kwamba kila mbunge anawakilisha taifa zima la Iran. Hii ina maana kwamba kazi kuu ya mwakilishi ni kuzingatia maslahi ya taifa. Ufuatiliaji bunge masuala ya eneo ufanyike katika mfumo wa mtazamo mkuu wa masuala ya nchi na uidhinishaji wa mipango ya maendeleo kwa njia iliyo sahihi na iliyo nje ya uwezo wa bajeti uepukwe.

Sherehe za ufunguzi wa muhula wa kumi na mbili wa Bunge la Iran, zimeanza Jumatatu hii asubuhi katika ukumbi wa umma wa Majlis kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wateule na maafisa wa kitaifa na kijeshi.

 

 

Tags