Uhusiano wa Iran na Qatar unaendelea kuimarika katika nyanja zote
Safari ya Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Qatar na kukutana kwake na Amir wa nchi hiyo kumefanyika katika mazingira ya kirafiki jambo linaloonyesha kuwa uhusiano wa Doha na Tehran unazidi kukua na kuimarika katika nyanja zote.
Hujjatul-Islamu wal-Muslimina Gholamhossein Mohseni Ejeei, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambaye ameitembelea Qatar siku ya Jumatano alikutana na kuzungumza na Tamim bin Hamad bin Khalifa Al-Thani, Amir wa Qatar. Katika Kikao hicho ambacho kilifanyika katika mazingira ya kirafiki pande zote zimejadili mambo mbalimbali yanayozihusu nchi mbili na matukio ya kieneo na kimataifa.
Nukta muhimu na ya kuvutia ya mkutano huo ni kwamba Mohseni Ejeei na Sheikh Tamim wameutaja uhusiano wa Iran na Qatar kuwa usio na matatizo na unaoendelea kuimarika katika nyuga mbalimbali na kutaka mwenendo huo udumishwe.
Katika kikao hicho Sheikh Tamim sambamba na kuelezea kufurahishwa kwake na uwepo wa Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Qatar, ameutaja uhusiano wa nchi hizi mbili kuwa wa kistratijia na usio na matatizo yoyote katika kipindi cha miongo minne iliyopita.
Mohseni Ejeei aidha ameeleza kuwa, kiwango cha uhusiano kati ya Iran na Qatar katika nyuga mbalimbali hususan katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kimekuwa kikiendelea na kustawi, na kutaka mwenendo huo udumishwe.
Jambo lingine muhimu ni kwamba pande hizi pia zimetumia diplomasia ya mahakama kupanua uhusiano wao. Kwa hakika, diplomasia ya mahakama imethibitisha kuwa uhusiano kati ya Qatar na Iran ni zaidi ya uhusiano wa kawaida wa nchi mbili.
Kuhusiana na hilo, mkuu wa mfumo wa mahakama wa Iran amezungumzia haja ya kustawishwa uhusiano wa kisheria na kimahakama kati ya Iran na Qatar hususan katika uga wa kusamehewa na kubadilishana wafungwa kwa kuzingatia kukaribia sikukuu ya Eidi Al-Adha. Kuhusiana na hilo, Ejeei amemwomba Amir wa Qata aruhusu idadi ya wafungwa wa Iran wanaoshikiliwa nchini humo warejeshwe Iran ombi ambalo limekubaliwa na Amir huyo.
Nukta nyingine ni kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Qatar ni nchi mbili ambazo zina nafasi kubwa katika kuunga mkono suala la Palestina na Ukanda wa Gaza. Serikali ya Qatar inafanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuupatanisha utawala wa Kizayuni na Hamas ili kufikia usitishaji vita wa kudumu na kumaliza vita huko Gaza.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia inajaribu kuelekeza maoni ya waliowengi duniani katika uzingatiaji wa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza kupitia vikao vya kieneo na kimataifa. Katika kikao baina ya Amir wa Qatar na mkuu wa vyombo vya mahakama vya Iran, Mohseni Ajeei ameshukuru misimamo ya Amir na serikali ya Qatar kuhusu suala la Ukanda wa Gaza na kusema, ni muhimu kwa nchi za Kiislamu kuchukua hatua za dharura kwa ajili ya kupunguza mateso ya watu wa ukanda huo, kukomesha jinai na kufuatilia kisheria uhalifu wa vita unaofanywa na watawala wa Israel.
Mbali na masuala yaliyotajwa, Qatar na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima zimekuwa zikijaribu kusaidiana katika matatizo mbalimbali. Kwa mfano, mwaka 2017, wakati Qatar ilizingirwa na nchi 4 za Kiarabu na kukabiliwa na hali ngumu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisaidia nchi hiyo kuondokana na hali hiyo, na kwa upande wake, Qatar nayo imekuwa na nafasi muhimu katika upatanishi kati ya Iran na nchi za Magharibi, hasa katika kufikisha jumbe za pande hizo katika upande wa pili. Hivyo tunaweza kusema kuwa uhusiano wa Iran na Qatar ni kielelezo chema cha kuigwa katika mahusiano ya pande mbili kati ya nchi za eneo.