Jun 16, 2024 12:49 UTC
  • Iran yakosoa taarifa ya G7, yasisitiza italinda usalama wake kwa nguvu zote

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kufanya hima kuhakikisha kuwa usalama endelevu unazidi kuwepo katika eneo la Asia Magharibi.

Nasser Kan'ani amesema hayo leo Jumapili, ambapo sambamba na kukosoa taarifa ya kundi la G7, amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itafanya kila liwezekanalo kulinda usalama na maslahi ya taifa hili.

Mwishoni mwa mkutano wa siku mbili wa kundi la nchi saba zilizostawi zaidi kiuchumi duniani, G7 iliionya Iran eti isifanye chokochoko za nyuklia, na itoe dhamana kwamba mradi wake wa nyuklia unaendana na azimio la Juni 5 la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Atomiki IAEA.

Aidha jumuiya hiyo ya kiuchumi imeituhumu Iran kuwa inasaidia Russia katika vita vya Ukraine, huku ikitishia kuichukulia Tehran 'hatua' iwapo itatekeleza makubaliano ya kuipa Moscow makombora ya balestiki.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitiza kuwa, mradi wa nyuklia wa Iran una malengo ya amani, na hilo limethibitishwa na IAEA.

Aidha ameeleza bayana kuwa, hatua ya G7 ya kuashiria azimio la Bodi ya Magavana ya IAEA inaonyesha kuwa azimio hilo lilikuwa la kisiasa, na kusisitiza kwamba madola ya Magharibi yanatumia taasisi za kimataifa kuyashinikiza mataifa huru.