Kaimu Rais wa Iran alaani uhalifu wa Israel huko Gaza, kimya cha jamii ya kimataifa na nchi za Waislamu
Kaimu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu, Mohammad Mokhber, amelaani vikali jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza huku kukiwa na kimya cha taasisi za kimataifa na nchi za Kiislamu.
Mokhber amesema: "Katika siku za hivi karibuni, uhalifu wa Wazayuni huko Gaza umeongezeka kwa kuungwa mkono na Marekani, na juhudi zote za kimataifa za usitishaji vita pia zimeshindwa."
Kaimu Rais wa Iran ameongeza kuwa, hali mbaya na isiyo ya kibinadamu huko Gaza imeacha "doa lingine la aibu" katika rekodi mbaya ya jinai ya utawala wa Israel.
Mokhber pia amezikosoa nchi za Kiislamu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao na kutochukua hatua yoyote ya kivitendo ya kuwatetea watu wa Gaza.

Matamshi hayo ya Kaimu Rais wa Irani yamekuja wakati Israel inaendelea kushambulia makazi ya raia, shule, na vituo vya shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina, UNRWA, katika eneo lililozingirwa na vita na mauaji ya kimbari la Gaza.
Siku ya Jumamosi, ndege za kivita za F16 za Israel zilishambulia eneo la al-Mawasi kusini mwa Gaza na kuua shahidi Wapalestina wasiopungua 90. Raia wengine 300 walijeruhiwa.
Mapema jana Jumapili pia, jeshi la Israel lilishambulia shule inayosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi na Ajira kwa Wapalestina (UNRWA) katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat na kuua watu wasiopungua 15. Wapalestina wengine 80 wamejeruhiwa.