Sisitizo la China la kuunga mkono mamlaka ya kitaifa ya Iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China Wang Yi anasema Beijing inaiunga mkono Iran katika kutetea "mamlaka yake, usalama na heshima ya taifa" huku Tehran ikiahidi kuiadhibu vikali Israel kutokana na mauaji ya aliyekuwa Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.
Wang Yi amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigenii wa Iran Ali Bagheri Kani siku ya Jumapili, na kusisitiza kwa mara nyingine msimamo wa Beijing wa kulaani mauaji ya mkuu wa Hamas jijini Tehran mwishoni mwa mwezi uliopita.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China imesema katika taarifa yake kwamba, wakati wa mazungumzo hayo Wang Yi amesema, shambulizi lililopelekea kuuawa Haniyeh limekiuka mamlaka ya kujitawala ya Iran na kuwa tishio kwa uthabiti wa eneo hilo
Aliongeza kuwa mauaji ya Haniyeh "yamedhoofisha moja kwa moja mchakato wa mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza na kutoa pigo kwa amani na utulivu wa kikanda."
Kuhusiana na hilo, Ali Sharifinia, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema:
"Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaona ni wajibu kulipiza kisasi cha damu ya mgeni wake mpendwa. Aidha, inaamini kuwa iwapo Wazayuni hawatapewa jibu kali, wataendelea kuhatarisha usalama wa taifa na eneo kwa kuendeleza jinai zao, na hilo litageuka na kuwa mazoezi hatari.
Katika fremu hiyo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China imetangaza kuwa, Wang Yi alimwambia Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran kwamba kuuawa shahidi Haniyeh kumeliidhoofisha moja kwa moja mchakato wa mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza na kuhatarisha amani na utulivu wa eneo hili.
Nchi kama China, ambayo ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ina jukumu zito la kuzuia kuendelea maovu ya utawala mtenda jinai wa Kizayuni, na haipaswi kuruhusu utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, uhatarishe usalama wa kikanda na kimataifa. Ni kwa sababu hiyo ndio maana, hivi karibuni China ilianza kutekeleza sera amiilifu zaidi katika kusaidia kutatua mzozo wa Asia Magharibi. Juhudi za Beijing za kuleta umoja wa kitaifa kati ya makundi ya Wapalestina zinahesabiwa kuwa miongoni mwa hatua athirifu na za kujenga za China katika suala hili.
Wakati huo huo, uungaji mkono wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China kwa haki ya Iran ya kutetea na kulinda mamlaka yake ya kitaifa dhidi ya maovu ya Wazayuni unaonyesha pia ukweli kwamba, China kwa mujibu wa uzito wake wa kimataifa ikiwa ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa inajaribu kuwa na taathira kwa mahesabu na milinganyo ya kikanda na kimataifa.
Kinyume na hivyo, utawala wa Kizayuni utaendelea kukariri jinai zake kwa kiburi na hivyo kuhatarisha usalama wa eneo hili. Ukweli ni kwamba China pia imefikia hitimisho kwamba, iwapo hatua madhubuti za kieneo na kimataifa hazitachukuliwa kumdhibiti mhalifu Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, utawala huo uutakuwa tishio kubwa kwa usalama wa kieneo na kimataifa, na hakuna mtu au nchi ambayo itasalimika na hilo.
China, ikiwa ni taifa kubwa la mashariki, huku ikitetea haki za kimataifa za mataifa, inaweza kuongeza mashinikizo ya kisiasa kwa utawala wa Kizayuni. Hii ina maana kuwa, nchi zilizoungana za Mashariki au Kusini mwa dunia zinaweza kuzuia kuendelea ushari na maovu ya Wazayuni huko Gaza na katika eneo hili kwa kuimarisha ushirikiano wao na kuchukua hatua za kimsingi.