Aug 14, 2024 02:22 UTC
  • Kukanushwa tuhuma za Marekani dhidi ya Iran

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema, Marekani ndiyo muungaji mkono na muenezaji mkuu wa ugaidi katika eneo na dunia.

Amir Saeed Iravani, ameyasema hayo katika barua aliyomwadikia Rais wa Baraza la Usalama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akijibu tuhuma za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba inaunga mkono ugaidi katika eneo na kubainisha kuwa, inachekesha na inaaibisha kwa Marekani kutoa tuhuma hizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati huohuo ikiwa inaunga mkono na kusaidia mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Israel, huku ikiwa mtetezi mkuu wa utawala huo.

Iravani amekanusha tuhuma hizo zisizo na msingi na kulaani mienendo ya kutowajibika ya mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa na kueleza kwamba, misaada ya silaha ya Marekani kwa Wazayuni ni kwa ajili ya kuendeleza mauaji ya Wapalestina wasio na hatia wakiwemo watoto na wanawake.

Ameongeza kuwa, jinai ya karibuni zaidi ya utawala wa Israel dhidi ya raia wasio na makazi katika Skuli ya Al-Tabeen katikati ya mji wa Gaza mnamo Jumamosi, Agosti 10, 2024, ambayo ilipelekea kuuawa shahidi Wapalestina wasio na hatia wasiopungua 100, wakiwemo watoto na wanawake, ni matokeo ya uungaji mkono huohuo wa Marekani usio na udadisi wowote.

 

Katika muda wote wa kikao hicho, mwakilishi wa Marekani akijibu matamshi ya mwakilishi wa Russia, akikengeuka ajenda ya kikao hicho, alitoa tuhuma zisizo na msingi, za upotoshaji na za uwongo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na uungaji mkono wa ugaidi katika eneo hili.

Tukitupia jicho matukio ya kikanda na kimataifa na matukio ya vurugu na utumiaji mabavu, inafahamika  wazi kabisa kwamba, ni nchi na tawala zipi zinazosababisha matatizo na mivutano ya kimataifa. Hata hivyo, kutokana na uwezo wake wa vyombo vya habari na ushawishi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani inafuatilia kupotosha mambo.

Ali Jamali, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema:

"Kila kona ya dunia, tunaweza kuona kwa urahisi athari za maovu ya Marekani. Ukweli ni kwamba Marekani inatumia wenzo wa ushari na uzushaji mivutano ili kuendeleza malengo yake maovu. Marekani imekuwa ikifanya njama za kuhalalisha uwepo wake wa kijeshi katika maeneo mbalimbali ya dunia kwa kutumia kisingizio cha kushughulikia migogoro na kukabiliana na ukosefu wa usalama. Kwa msingi huo, shutuma za Marekani zimekuwa hazina maana kabisa kwa walimwenguu kwani hadaa yake hiyo imeshafahamika.

Tukitupia jicho chimbuko la mgogoro wa Ukraine na kupigana vita nchi hiyo na Russia inafahamika wazi kwamba, msababishaji wa mgogoro na vita hiyo ni Marekani, na inaendelea kuchochea ukosefu wa usalama na mgogoro katika maeneo tofauti kwa kusisitiza upanuzi wa kijiografia wa NATO. Matukio ya Afghanistan, kuendelea ugaidi katika nchi hiyo sambamba na himaya na uungaji mkono kwa jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni wa  Israel huko Gaza, ni sehemu tu ya uovu na kuendelezwa siasa za utumiaji mabavu za Washington katika maeneo tofauti ya dunia.

Magaidi wa Daesh nchini Afghanistan

 

Kwa kupinga rasimu kadhaa za azimio la kusitisha mapigano huko Gaza kwa kutumia kura ya veto, Marekani inasaidia kuendelea jinai za Wazayuni. Wakati huo huo, wataalamu wote wa kimataifa wamekiri kwamba, utawala wa Kizayuni unaweza tu kuendelea kuwaua watu wa Gaza kwa uungaji mkono kamili wa Marekani. Kwa kuanzisha kundi la kigaidi la Daesh, Marekani ilifanya ukatili na viitendo vingi visivyo na idadi Iraq na Syria, na kuua mamia ya maelfu na kujeruhi mamilioni ya wengine. Filihali kwa kuhamishia magaidi wa Daesh huko Afghanistan, Marekanii imo mbioni kuanzisha maovu nchini Afghanistan na kuhamisha ugaidi hadi Asia ya Kati na kwenye mipaka ya Uchina.

Pamoja na kuwa Marekani ina faili kama hilo lililojaa uovu na ukatili, lakini viongozi wa nchi hiyo wakiwa na jeuri kamili wanatoa tuhuma za kigaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  Kwa kufanya hivyo, Marekani inafuatilia malengo kadhaa.

Mosi ni kuwa, viongozi wa Marekani wanataka kufunika uhalifu wao. Pili, wanajaribu kupotosha fikra za waliowengu na kuzifanya zisizingatie jinai zake na za Israel. Na tatu ni kuwa, Marekani daima imekuwa ikijaribu kuzuia upatikanaji wa maafikiano ya kulaani vitendo vyake vya kigaidi na utawala ghasibu wa Israel kwa kuibua masuala ya uongo katika mikutano ya kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa.