Aug 18, 2024 02:59 UTC
  • Iran: Tuna haki ya kujibu mapigo ya mauaji ya kigaidi ya Haniyah

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ina haki ya kujibu kwa njia halali kitendo cha utawala wa Kizayuni wa Israel cha kumuua kigaidi Ismail Haniyah, aliyekuwa Kiongozi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas akiwa ziarani hapa mjini Tehran.

Ali Bagheri Kani alisema hayo jana katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty na kuongeza kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki yake ya asili na halali ya kujibu kihalali jinai ya utawala wa Kizayuni."

Ameeleza bayana kuwa, "Watu wa Palestina hawatasalimu amri mbele ya utawala wa Kizayuni kutokana ujasiri wao wa kupigiwa mfano. Tel Aviv inafanya jinai katika medani, na hadaa kupitia mazungumzo."

Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran vile vile ameikashifu Washington kwa kuunga mkono utawala wa Kizayuni katika vita vyake dhidi ya Gaza na kusema kuwa, Marekani haiwezi kuwa mpatanishi asiyeegemea upande wowote katika mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza kutokana na uungaji mkono wake usio na kifani, ambao unaifanya Washington kuwa mshiriki wa jinai dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Kwa upande wake, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mivutano katika eneo la Asia Magharibi, na kutoa mwito wa kuchukuliiwa hatua za kutuliza hali na kupunguza kiwango cha mivutano kwa kuzingatia masilahi ya pande zote.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Misri ameashiria duru mpya ya mazungumzo yenye lengo la kutaka kufikiwa makubaliano usitishaji vita huko Gaza, ambayo yalifanyika katika mji mkuu wa Qatar, Doha kwa upatanishi wa Marekani, Misri na Qatar na kusema kuwa, Misri inafanya juhudi kuwasaidia watu wa Palestina na kusaidia kukomesha mara moja jinai za Israel huko Gaza.

Tags