Aug 31, 2024 04:16 UTC
  • Iran: Uingereza inaendeleza siasa za kindumilakuwili kuhusu ugaidi

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini London umeilaumu Uingereza kwa siasa zake za nyuso mbili kuhusu ugaidi na kusema kuwa, wakati wananchi wa Iran wanapouawa kigaidi, kwa mujibu wa serikali ya London, ugaidi huo unavumilika, na hauwezi kuchukuliwa msimamo kama wa ugaidi unaofanyika maeneo mengine.

Kwa mujibu wa IRNA, Ubalozi wa Iran mjini London, Uingereza umetuma ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa X na kuandika kuwa, tarehe 30 Agosti 1981, Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliuliwa kigaidi na genge la wanafiki la MKO, genge ambalo kwa muda mrefu jamii ya kimataifa ilikuwa ikilitambua kuwa ni la kigaidi, lakini inashangaza kuona kuwa Uingereza hailitambui genge hilo kuwa ni la kigaidi.

Sehemu nyingine ya ujumbe huo imesema, Uingereza hailitambui genge la MKO kuwa ni la kigaidi kwa sababu inataka kuiweka chini ya mashinikizo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baadhi ya wabunge wa Uingereza wanachukua misimamo ya kiuadui kupindukia dhidi ya Iran kiasi kwamba kila mwaka wanamkaribisha nchini Uingereza mkuu wa genge hilo la kigaidi na wanashirikiana na baadhi ya magazeti yenye historia chafu na majina mabaya kuunga mkono vitendo vya kigaidi vya genge hilo.

Rais na Waziri Mkuu wa Iran waliouliwa kigaidi na genge la MKO tarehe 30 Agosti 1980. Genge hilo la kigaidi la MKO hadi leo linafadhiliwa na madola ya Magharibi ikiwemo Uingereza

 

Shahid Mohammad Ali Rajai, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu, na Hujjatul Islam Walmuslimin Mohammad Javad Bahonar aliyekuwa Waziri Mkuu wa Iran, waliuawa shahidi kigaidi tarehe 30 Agosti 1981 katika shambulio la bomu lililotengwa na magaidi wa MKO kwenye ofisi ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iran.

Jana Ijumaa ilikuwa ni siku ya kukumbuka kuuawa shahidi viongozi hao wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu, siku ambayo hapa Iran inatambuliwa kwa jina la Siku ya Taifa ya Kupambana na Ugaidi.

Tags