Rais wa Iran kuelekea Qatar kesho Jumatano
Rais wa Iran kesho Jumatano ataondoka hapa Tehran na kuelekea Qatar kwa madhumuni ya kushiriki katika kikao rasmi cha nchi mbili na kushiriki katika Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia.
Rais Masoud Pezeshikian ataelekea Qatar hiyo kesho akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa kisiasa na kiuchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mbali na kukutana na kufanya mazungumzo ya pande mbili, Rais Pezeshkian atashiriki pamoja na Amir wa Qatar katka vikao vya ngazi ya juu vinavyohusu masuala ya nchi mbili na katika hafla ya kutia saini hati za ushirikiano wa pamoja kati ya nchi mbili. Ziara hiyo ya siku mbili ya Rais wa Iran nchini Qatar, inafanyika kwa mwaliko rasmi wa Amir wa nchi hiyo, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani.
Katika siku ya pili ya safari yake nchini Qatar, Dakta Pezeshkian atashiriki na kutoa hotuba katika mkutano wa 19 wa Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD) na pia atakuwa na mikutano na baadhi ya viongozi na maafisa wa nchi zinazoshiriki katika jukwaa hilo.
Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD) ambalo lina nchi wanachama 22 ndilo kongamano kubwa zaidi la Asia ambalo lilianzishwa mwaka 2002 kwa lengo la kuendeleza ushirikiano wa kuitamaduni, kiuchumi na kijamii.