'Makombora ya Iran ya kizazi kipya yatashangaza ulimwengu, yako tayari kurushwa'
Kamanda wa zamani katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ambaye sasa ni mbunge amesema makombora ya Iran ya kizazi kipya yako tayari kuvurumishwa ili kutoa jibu thabiti na kali kwa shambulio lolote linaloweza kufanywa na Israel kufuatia operesheni ya kulipiza kisasi ya Operesheni ya Ahadi ya Kweli II dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Mohammad Esmaeil Kowsari amesema: “Maeneo ya kuvurumishia makombora yako tayari kujibu kitendo chochote cha uovu kinachoweza kufanywa na utawala wa Kizayuni. Ulinzi wa anga wa nchi yetu kwa sasa uko katika kiwango chake cha juu zaidi cha utayari."
Aidha amesema Iran bado haijaanza kutumia makombora yake ya kiwango cha juu huku akiongeza kuwa: "Iwapo kutakuwa na uchokozi wowote, kwa mara ya kwanza tutatumia makombora hayo, ambayo nguvu zake za uharibifu zitashangaza dunia nzima.”
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Jumanne usiku lilitoa taarifa likitangaza kuwa limeshambulia kitovu cha maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina (Israel) ikiwa ni katika kujibu mauaji ya shahidi Ismail Haniya, Sayyid Hassan Nasrullah na Meja Jenerali Abbas Nilforoushan Kamanda na mshauri wa ngazi ya juu wa IRGC huko Lebanon. Oparesheni hiyo kwa jina la Ahadi ya Kweli ya Pili imetekelezwa kwa idhini ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na baada ya kujulishwa kamandi kuu ya vikosi vya ulinzi na kuungwa mkono na jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wizara ya Ulinzi.