Mwalimu Muirani auawa nchini Ujerumani
Vyombo vya habari vya Ujerumani vimetangaza kuwa mwalimu mmoja Muirani ameuawa katika mazingira ya kutatanisha katika mji wa Celle nchini humo.
Habari zinasema kuwa, maiti ya Mahdi J. aliyekuwa na umri wa miaka 55 na mwalimu katika shule moja ya sekondari ya mji wa Celle kwenye jimbo la Niedersachsen (Lower Saxony) nchini Ujerumani ilikutwa nyumbani.
Ripoti zinasema kuwa, polisi ya Ujerumani ambayo hadi sasa haijajua muuaji au wauaji wa mwalimu huyo Muirani, imeunda kamati maalumu ya kuwafutilia wahusika wa mauaji hayo.
Matokeo ya uchunguzi wa maiti ya Mahdi J. yanaonesha kuwa kifo chake kilisababishwa na kupigwa kichwani.
Uchunguzi wa awali wa polisi ya Ujerumani umeonesha kuwa, Muirani huyo alikuwa mtu mwema aliyependa sana kusaidia wanadamu wengine na kwamba aliwahi kwenda kwenye kambi za wakimbizi kwa hiari yake kutoa msaada ukalimani. Habari zinazema kwamba wakati mwingine alikuwa akiwapa hifadhi wakimbizi nyumbani kwake.
Polisi ya Ujerumani inawashuku vijana wawili ambao siku ya mauaji ya mwalimu huyo Muirani walionekana karibu ya nyumba yake.