Pezeshkian: Hatuhitaji Magharibi kulinda usalama wa eneo hili
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i121628-pezeshkian_hatuhitaji_magharibi_kulinda_usalama_wa_eneo_hili
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Iran na Russia kwa kushirikiana vizuri zinaweza kufuata sera huru na kudhamini usalama wa kisiasa na kiuchumi wa eneo hili.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jan 19, 2025 02:44 UTC
  • Pezeshkian: Hatuhitaji Magharibi kulinda usalama wa eneo hili

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Iran na Russia kwa kushirikiana vizuri zinaweza kufuata sera huru na kudhamini usalama wa kisiasa na kiuchumi wa eneo hili.

Rais Pezeshkian ambaye karibuni hivi alifanya safari mjini Moscow kwa ajili ya kutia saini makubaliano ya kina ya ushirikiano wa kimkakati na Russia, siku ya Ijumaa baada ya kukutana na mwenyeji wake Rais Vladimir Putin, alifanya mahojiano na Kanali ya Kwanza ya televisheni ya nchi hiyo, ambapo aligusia masuala muhimu ya kieneo na kimataifa.

Katika mazungumzo hayo Pezeshkian ameeleza kuwa nchi hizi mbili zina uwezo wa kutekeleza sera ya kujitegemea na ziko tayari kuhakikisha amani na usalama wa kiuchumi unadumishwa katika ukanda huu kwa kushirikiana baina yao kwa lengo la kuleta amani na utulivu katika eneo.

Huku akiashiria kwamba kutiwa saini makubaliano mapya ya kistratijia kati ya Iran na Russia ni ishara ya upinzani wa nchi hizo dhidi ya siasa za nchi za kigeni, Rais wa Iran amesema: Iran na Russia hazizihitajii nchi za Magharibi.

Ikumbukwe kuwa kwa kutiwa saini makubaliano ya kina ya kistratijia kati ya Iran na Russia, nchi hizo mbili zitapanua uhusiano wao kwa namna maalum katika nyanja za kiuchumi, kisayansi, kiteknolojia, kiutamaduni na kitalii.