Iran yapongeza hatua ya Afrika Kusini ya kuishtaki Israel ICJ
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i122700-iran_yapongeza_hatua_ya_afrika_kusini_ya_kuishtaki_israel_icj
Mansour Shakib Mehr, balozi wa Iran nchini Afrika Kusini amepongeza hatua ya serikali ya Pretoria ya kuwasilisha mashtaka dhidi ya utawala haramu wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) kutokana na jinai za utawala huo ghasibu huko Gaza.
(last modified 2025-02-13T23:03:04+00:00 )
Feb 13, 2025 23:03 UTC
  • Iran yapongeza hatua ya Afrika Kusini ya kuishtaki Israel ICJ

Mansour Shakib Mehr, balozi wa Iran nchini Afrika Kusini amepongeza hatua ya serikali ya Pretoria ya kuwasilisha mashtaka dhidi ya utawala haramu wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) kutokana na jinai za utawala huo ghasibu huko Gaza.

Akihutubia katika hafla ya kumbukumbu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran iliyofanyika mjini Pretoria na kuhudhuriwa na shakhsia mbalimbali wa kiserikali na Wairani wanaoishi nchini humo, balozi Mansour Shakib Mehr sambamba na kuzungumzia uhusiano mzuri baina ya mataifa haya mawili aliipongoza serikali ya nchi hiyo kwa hatua yake ya kuwasilisha kesi katika mahakama ya ICJ dhidi ya utawala vamizi wa Israel.

Mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka 2023, Afrika Kusini iliwasilisha malalamiko katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu dhidi ya utawala wa Kizayuni kutokana na utawala huo kukiuka makubaliano ya kupigwa marufuku jinai za mauaji ya kimbari.

Aidha  Novemba mwaka jana (2024) Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitoa waranti wa kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na aliyekuwa waziri wake wa vita Yoav Gallant baada ya kuwafungulia mashtaka ya kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Gaza, ambako utawala wa Kizayuni uliendesha vita vya kinyama vya miezi 15 na kufanya mauaji ya kimbari tangu mwezi wa Oktoba mwaka 2023.

Afrika Kusini imeapa kutoondoa kesi yake ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), licha ya vitisho, mashinikizo na kukatiwa misaada na utawala wa Donald Trump.