Iran yalaani shambulizi la kigaidi la Balochistan, Pakistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali shambulio la kigaidi katika jimbo la Balochistan nchini Pakistani, ambalo limesababisha vifo na kujeruhiwa wafanyakazi kadhaa wasio na hatia.
Ismail Baghaei, amelaani vikali shambulio hilo la kigaidi lililotokea karibu na mgodi wa makaa ya mawe huko Harnai, Balochistan, Pakistan, jana Ijumaa, Februari 14, 2025, na kusababisha vifo na kujeruhiwa wafanyakazi wa mgodi huo waliokuwa wanajitafutia riziki zao za halali.
Akitilia mkazo msimamo usiotetereka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kulaani ugaidi wa aina zote na popote pale unapotokea, Baghaei ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga, wananchi na serikali ya Pakistan na kuwatakia afueni ya haraka majeruhi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Iran pia amesisitizia haja ya kuimarishwa juhudi na ushirikiano baina ya pande mbili na pia ushirikiano wa nchi zote za ukanda huu katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi.
Tukio hilo lilitokea jana Ijumaa, Februari 14, baada ya gari lililokuwa limebeba wachimba migodi kuripuliwa kwa bomu katika mji wa Harnai, Pakistan. Polisi wa mkoa wa Balochistan ya Pakistan wamethibitisha tukio hilo na kusema kuwa, wafanyakazi wasiopungua 11 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Hadi wakati tunaandaa habari hii hakukuwa na kundi lolote lililodai kuhusika na mripuko huo. Lakini genge la kigaidi linalotaka kujitenga linalojulikana kwa jina la Baloch Liberation Army huwa mara kwa mara linadai kuhusika na mashambulizi mengi ya kigaidi kwenye eneo hilo.