Iran yalaani kufutwa mkutano wa Geneva wa kuijadili Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i123732-iran_yalaani_kufutwa_mkutano_wa_geneva_wa_kuijadili_palestina
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amekosoa vikali uamuzi wa Uswisi wa kufuta Kongamano la Hati ya Geneva kuhusu Palestina.
(last modified 2025-03-10T07:51:07+00:00 )
Mar 10, 2025 07:51 UTC
  • Iran yalaani kufutwa mkutano wa Geneva wa kuijadili Palestina

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amekosoa vikali uamuzi wa Uswisi wa kufuta Kongamano la Hati ya Geneva kuhusu Palestina.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu asubuhi, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema kuwa Uswisi, kama mlinzi na mlezi wa mikataba ya kimataifa ya sheria za kibinadamu-hasa Mikataba Minne ya Geneva ya 1949-ilitarajiwa iunge mkono ulinzi wa raia na miundombinu ya kiraia katika migogoro ya silaha.

Mkutano huo uliopangwa kufanyika Machi 7, ulilenga kuzileta pamoja nchi zilizopasisha azimio la kuimarisha sheria ya kimataifa ya kibinadamu katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, hususan huko Gaza.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema uamuzi wa Uswisi wa kuufuta mkutano huo umepokelewa kwa masikitiko na mshangao mkubwa.

Ameeleza bayana kuwa, suala hilo pia lilijadiliwa wakati wa mkutano wa hivi karibuni wa Jeddah, ambapo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) walielezea kusikitishwa na kufutwa kwa mkutano huo.