Iran: Kumetolewa wazo jipya la kutatua masuala ya nyuklia na IAEA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametangaza kuwa, Tehran inalichunguza wazo jipya la kutatua masuala ya nyuklia ya Iran kati ya Tehran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.
Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo kwenye mahojiano na gazeti la Iran, toleo la leo asubuhi na kutetea ushirikiano amilifu na pande mbalimbali ulimwenguni kwa sharti kwamba mazungumzo hayo yazingatie kanuni za kimsingi za "heshima, hekima na ustahiki."
Aidha amesema: Mkakati wa Iran wa subira hauendeshwi kwa pupa bali ni subira iliyoambatana na idili, umakini na ubunifu.
Sayyid Araghchi amegusia pia jibu la Iran kwa sera ya mashinikizo ya juu kabisa ya rais wa Marekani, Donald Trump na kusema: "Mazungumzo hayatazaa matunda yoyote ya maana kwani upande wa pili wa mazungumzo hayo unazidi kuweka mashinikizo ya juu kabisa. Ili kujibu mashinikizo hayo, upande wa pili nao unafanya kadiri uwezavyo kuthibitisha kwamba sera ya mashinikizo haina maana yoyote. Inabidi hilo lifanyike kivitendo ili ipatikane fursa ya kuketi kwenye meza ya mazungumzo kwa kuheshimiana."
Akikumbushia upatanishi wa nchi za Ulaya katika mapatano ya JCPOA, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Wazungu walikuwa na nafasi nzuri ya upatanishi katika duru iliyopita, hivi sasa pia wanaweza kuwa na nafasi nzuri ya upatanishi na ndio maana mazungumzo ya Iran na nchi za Ulaya yataendelea, lakini hatima ya yote ni kwamba Marekani lazima iondoe vikwazo ilivyoweka ili mazungumzo ya kuheshimiana yaanze, bila ya shinikizo wala vitisho."