Iran: Tunataka makubaliano ya haki, heshima na usawa; Israel yaingiwa na kiwewe
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema Jamhuri ya Kiislamu inataka makubaliano ya haki na ya heshima, na yaliyojadiliwa kwenye mazingira ya usawa. Sayyid Araghchi amesema hayo kabla ya kuanza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na wawakilishi wa Marekani.
Akizungumza baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr bin Hamad Al Busaidi mjini Muscat leo Jumamosi, Araghchi amesema ikiwa Marekani ina dhamira ya kweli, pande hizo mbili zinaweza kuamua ratiba ya mazungumzo hayo.
"Nia yetu ni kufikia makubaliano ya haki na yenye heshima, na yalifokiwa katika mazingira ya usawa," amesema. Waziri Araghchi amesema iwapo upande wa pili utafika kwenye meza ya mazungumzo kwa mtazamo huo huo, kutakuwa na nafasi ya maelewano ya awali ambayo yataashiria njia ya kuendelea kwa mazungumzo.
Wanadiplomasia wakuu wa Iran na Oman wamekutana mjini Muscat kabla ya kuanza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na ujumbe wa Marekani, ambayo yanalenga kusitisha vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mpango wa nyuklia wenye malengo ya kiraia wa nchi hii.
Mapema leo Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na mwenzake wa Oman walikubaliana kuhusu utaratibu wa mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja.
Kadhalika Araghchi ameelezea kuridhishwa kwake na uhusiano thabiti na wa muda mrefu kati ya Tehran na Muscat, huku akisifu mtazamo wa uwajibikaji wa Oman katika masuala na maendeleo ya kikanda, na akasisitiza kuwa, Oman, kama mwenyeji wa mazungumzo ya moja kwa moja ya Iran na Marekani ni ushuhuda wa sera hiyo.
Wakati huo huo, imefichuka kuwa, utawala haramu wa Israel unaendesha kampeni kubwa ya hujuma ya kisaikolojia dhidi ya mazungumzo hayo ya Oman kati ya Iran na Marekani kupitia njia mbalimbali.
Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa kanali ya televisheni ya Al-Alam, chanzo kinachofahamu mchakato wa mazungumzo hayo kimepuuzilia mbali uvumi kwamba suala la kulipiza kisasi mauaji ya kigaidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), litaibuliwa katika mazungumzo hayo.
Chanzo hicho ambacho hakikutajwa jina kimesisitiza kuwa, masuala hayo hayajawasilishwa na upande wa Marekani, si katika taarifa zao rasmi au zisizo rasmi. Hii ni katika hali ambayo Iran imeapa kufuatilia kesi hiyo kupitia njia za kisheria za kimataifa.