Iravani: Iran ni mmiliki wa visiwa vitatu katika maji ya Ghuba ya Uajemi
-
Amir-Saeid Iravani
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amekanusha madai ya Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi kwamba Iran inaingilia mamlaka ya visiwa vya Boumousi, Tunb Kubwa na Tunb Ndogo katika Ghuba ya Uajemi na kuyataja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa kanuni na sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Akijibu tuhuma zisizo na msingi zinazotolewa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama katika Baraza la Ushirikiano wa Ghuba wa Uajemi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Amir-Saeid Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa Iran ndio yenye mamlaka ya visiwa hivyo vitatu na kutangaza kwamba madai yoyote kinyume na hivyo ni "uingiliaji usiokubalika."
Iravani pia amepinga "jina bandia" linalotolewa kwa eneo la Ghuba ya Uajemi, na kusema kwamba jina "Ghuba ya Uajemi" ni jina la kihistoria na la kisheria la mkondo huo wa bahari, ambalo limetumika kwa muda mrefu katika hati za kimataifa na maandishi ya kihistoria.
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu, siku zote imekuwa ikitilia mkazo kanuni za sheria za kimataifa ikiwemo kanuni ya usawa wa nchi zinazojitawala na ujirani mwema, na sera yake ya kuimarisha utulivu na kuendeleza amani ya eneo la Magharibi mwa Asia inatokana na msimamo wa kuheshimiana na mazungumzo yenye kujenga na majirani wote wa Ghuba ya Uajemi.