Araqchi: Nimeridhishwa na hatua zilizopigwa katika mazungumzo na Marekani; mashauriano zaidi yanahitajika
(last modified Sun, 27 Apr 2025 07:46:11 GMT )
Apr 27, 2025 07:46 UTC
  • Araqchi: Nimeridhishwa na hatua zilizopigwa katika mazungumzo na Marekani; mashauriano zaidi yanahitajika

Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema ameridhishwa na hatua zilizopigwa hadi sasa katika mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.

Araqchi ameeleza hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya duru ya tatu ya mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani kumalizika huko Muscat, mji mkuu wa Oman. 

"Nimeridhishwa na hatua zilizopigwa katika mazungumzo na kasi yake. Yanaendelea vizuri na yanaridhisha."

Ameongeza kuwa: Pande zote mbili zimedhamiria kufikia makubaliano. Ilikuwa dhahiri kwamba pande zote mbili zilikuwa jadi na ziliingia katika mazungumzo kwa dhamira ya dhati.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza kuwa pande mbili za Tehran na Washington zimekubaliana kufanya mashauriano zaidi katika miji mikuu ya nchi zao ili kupata njia za kutatua hitilafu zilizopo. 

"Zipo tofauti kati ya nchi mbili, na ni kuhusu masuala muhimu na mahsusi," amesema Araqchi. 

Kuna masuala ya hitilafu kati ya mataifa hayo mawili, katika masuala muhimu na mahususi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema duru ya nne ya mazungumzo itaongozwa na yeye na Steve Witkoff Mjumbe wa Rais Donad Trump kwa kuwajumuisha pia wataalamu wa pande zote mbili. 

Araqchi ameongeza kuwa wataalamu wa masuala ya uchumi walihudhuria kwa mara ya kwanza mazungumzo ya jana mjini Muscat, Oman, na kwamba wataalamu kutoka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) huenda wakashiriki duru ijayo ya mazungumzo.