Baqaei: Iran ina wasiwasi mkubwa kufuatia kuongezeka mzozo kati ya India na Pakistan
-
Esmail Baqaei
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Tehran ina wasiwasi mkubwa kufuatia kuongezeka mivutano kati ya India na Pakistan na amezitolea wito pande mbili kujizuia kuchukua hatua.
Esmail Baqaei ametilia mkazo msimamo mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu umuhimu wa kuheshimiwa mamlaka za kitaifa na umoja wa ardhi wa nchi mbalimbali.
Amesema, Tehran ina wasiwasi mkubwa kufuatia kuongezeka mvutano na mapigano kati ya nchi hizo mbili muhimu ambazo zimedumisha uhusiano wa kirafiki na wa muda mrefu na Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema anatumai kuwa India na Pakistan zitatoa kipaumbele kwa suala la kuacha kutumia nguvu ili kupunguza mvutano kwa lengo la kuzuia kuupa upande wa tatu, hususan utawala wa Israel, fursa ya kutumia vibaya hali hiyo.
Maafisa wa Pakistan wametangaza kuwa hadi sasa takriban watu 31 wameuawa na 46 kujeruhiwa katika mzozo unaoongezeka kati ya India na Pakistan.
Mvutano huo umekuwa ukiongezeka tangu Aprili 22 mwaka huu, kufuatia shambulio la kigaidi huko Pahalgam katika eneo la Jammu na Kashmir na kuuawa watu 26, huku Pakistan ikisema kuwa ipo tayari kwa uchunguzi wa kimataifa kuhusu hujuma hiyo.