Iran: Ripoti ya kituo cha nyuklia cha siri ni uzushi wa Netanyahu ili kuvuruga mazungumzo na Marekani
Iran imekanusha ripoti kuhusu kituo cha siri cha nyuklia, ikisema zimetolewa na kundi la kigaidi la MKO kwa agizo la waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa nia ya kuvuruga mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington.
Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi ametoa kauli hiyo kupitia chapisho kwenye X siku ya Ijumaa baada ya televisheni ya Fox News ya Marekani kusambaza ripoti ya kile ilichodai kuwa picha za setilaiti za kituo cha nyuklia kilichokuwa hakijulikani hapo awali katika Mkoa wa Semnan, Iran.
Araghchi amesema Netanyahu anatumia "vibaraka wa Kiiirani wa Saddam" chini ya sera yake ya kuamrisha nini Rais Donald Trump anatakiwa kufanya kuhusu Jamhuri ya Kiislamu, kwa jaribio la mwenye kutapatapa la kuvuruga mazungumzo ya Iran na Marekani.
Amesema: “Kama kawaida, 'Picha za Setilaiti za Kutisha' zinazosambazwa zinaongezeka wakati mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya nyuklia kati ya Iran na Marekani yanapokaribia kuanza tena."
Iran na Marekani tayari zimefanya duru tatu za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, yakisimamiwa na Oman, kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran na kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani.
Mapema Ijumaa, ujumbe wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa ulipinga ripoti hiyo ya Fox News na kuitaja kuwa "ya kipuuzi."
“Mbinu za kundi la kigaidi linalojulikana kama MKO zinaonyesha kwamba,katika jitihada za kupoteza matumaini ya kutambuliwa, linatoa ripoti za kubuni, zilizojificha kama taarifa za kijasusi, kwa mashirika ya kijasusi ya Magharibi, ikiwa ni pamoja na yale ya Marekani,” ulisema ujumbe huo katika taarifa iliyochapishwa kwenye X.
“Hata hivyo, pale mashirika kama hayo yanapogundua kutokuwa na uaminifu kwa ripoti za kipuuzi zinazotolewa na kundi la kigaidi la MKO, basi kundi hilo hutafuta wateja wapya miongoni mwa vyombo vya habari vya Magharibi, likilenga kutumia majukwaa hayo ili kupanda juu kwenye wimbi la umaarufu wa vyombo vya habari.”
Kundi la MKO, linalojulikana kwa ukatili wake, lina historia mbaya ya kufanya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya raia na maafisa wa Iran, na kuua takriban watu 12,000 tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.