Mtaalamu wa UN: Dunia iilazimishe Israel kusitisha mauaji ya kimbari Gaza
Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu amekemea vikali Israel kwa kuwachoma hai watu, hasa watoto, katika Ukanda wa Gaza, ambako utawala huo unaendesha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.
Francesca Albanese alitoa matamshi hayo kupitia chapisho kwenye mtandao wa X siku ya Jumatatu, baada ya shambulio la anga la Israel kuua kwa uchache watu 36, wakiwemo watoto 18, katika shule ya Fahmi al-Jarjawi mjini Gaza, ambako familia zilizokuwa zimekimbia mashambulizi zilikuwa zimekimbilia kutafuta hifadhi.
Waathiriwa wengi waliteketezwa kwa moto wakiwa wamelala kwenye hifadhi hiyo ya shule.
Video iliyorekodiwa katika eneo la tukio ilionyesha kivuli cha msichana mdogo akitembea kwenye vifusi akijaribu kujiokoa kutoka kwenye moto. Alinusurika katika mkasa huo, lakini alipoteza wanafamilia wake.
Albanese ameambatanisha video hiyo na chapisho lake, akisema: “Siwezi tena kuangalia moto bila kuhisi kichefuchefu tumboni.”
“Lazima tukomeshe mauaji haya ya kikatili," ameongeza. "Wapalestina na watusamehe."
Msemaji wa Uokoaji wa Raia wa Gaza, Mahmoud Basal, amesema shule hiyo ilipaswa kuwa “mahali pa usalama”, lakini “imegeuzwa kuwa Jahanamu.”
Amesema: “Tuliskia vilio vya maumivu kutoka kwa waliokuwa wamekwama ndani ya moto, lakini moto ulikuwa mkali mno. Hatukuweza kuwafikia."

Israel ilianzisha mashambulizi yake ya kinyama Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, baada ya harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, kufanya operesheni ya kihistoria dhidi ya utawala huo wa kikoloni, ikiwa ni kisasi kwa ukandamizaji uliokithiri dhidi ya watu wa Palestina.
Zaidi ya miezi 19 tangu mashambulizi hayo yaanze, utawala wa Tel Aviv bado umeshindwa kutimiza malengo yake iliyojiwekea yenyewe Gaza licha ya kuua Wapalestina wasiopungua 54,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine 122,966.
Israel imekuwa ikilenga mara kwa mara shule ambazo zimegeuzwa kuwa hifadhi za wakimbizi, jambo linalokiuka sheria za kimataifa za kibinadamu zinazokataza mashambulizi dhidi ya miundombinu ya raia.
Bila kutoa ushahidi wowote, jeshi la Israel lilidai kuwa shule ya Fahmi al-Jarjawi ilikuwa “kitovu cha uongozi na uratibu” wa makundi ya mapambano ya Hamas na Jihad Islami ya Palestina.