Ukuaji wa ajira duniani wapungua, Afrika na Amerika zaathirika zaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i126940-ukuaji_wa_ajira_duniani_wapungua_afrika_na_amerika_zaathirika_zaidi
Katika toleo lake jipya la Mtazamo wa Ajira na Kijamii duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la Ajira, ILO limebainisha kuwa mivutano ya kisiasa na hitilafu za kibiashara ni sababu kuu za kudhoofika kwa matarajio ya uchumi wa dunia, hali ambayo imesababisha kudorora kwa ukuaji wa ajira.
(last modified 2025-05-29T00:53:08+00:00 )
May 29, 2025 00:53 UTC
  • Ukuaji wa ajira duniani wapungua, Afrika na Amerika zaathirika zaidi

Katika toleo lake jipya la Mtazamo wa Ajira na Kijamii duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la Ajira, ILO limebainisha kuwa mivutano ya kisiasa na hitilafu za kibiashara ni sababu kuu za kudhoofika kwa matarajio ya uchumi wa dunia, hali ambayo imesababisha kudorora kwa ukuaji wa ajira.

Ikiwa imetolewa Jumatano huko Geneva, Uswisi, ripoti imepunguza makadirio ya awali ya ajira duniani kwa mwaka 2025, kutoka ajira mpya milioni 60 hadi milioni 53, ikimaanisha kuwa ukuaji wa ajira duniani umepungua kwa asilimia 0.2, huku pato la ukuaji wa pato la ndani la taifa, GDP nao ukikadiriwa kukua kwa asilimia 2.8, badala ya asilimia 3.2.

ILO inataja migogoro ya kibiashara hasa baina ya nchi tofuti za dunia na Marekani kuwa moja ya sababu za kupungua kwa ajira.

Mathalani inasema ajira zipatazo milioni 84 katika nchi 71 zinahusiana moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na mahitaji ya watumiaji bidhaa wa Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi za Afrika na Amerika ndizo zilizoathirika zaidi na upungufu wa ajira duniani. Ingawa viwango vya elimu vinaendelea kupanda duniani, soko la ajira bado linaathiriwa na kutolingana kwa elimu.

Kufikia mwaka 2022, ni asilimia 47.7 tu ya wafanyakazi ndio walikuwa na sifa zinazolingana ipasavyo na mahitaji ya kazi zao.

Ripoti hiyo pia inazungumzia athari za teknolojia mpya katika dunia ya ajira, ikionesha kuwa karibu mfanyakazi mmoja katika kila wafanyakazi wanne anaweza kuona kazi yake ikibadilika kutokana na Akili Mnemba ya kizazi kipya, GenAI.

Kazi za ujuzi wa kati ndizo zilizo na kiwango kikubwa cha uwezekano wa kuathirika, lakini kazi za ujuzi wa hali ya juu ndizo zilizo na uwezekano mkubwa zaidi wa majukumu yao kuweza kufanywa na AI.