Iran: Tuko tayari kuimarisha uhusiano na Ulaya lakini kwa kuheshimiana
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i127352-iran_tuko_tayari_kuimarisha_uhusiano_na_ulaya_lakini_kwa_kuheshimiana
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesema kuwa, Tehran iko tayari kupanua uhusiano na nchi za Ulaya hususan Italia lakini kwa sharti la kuheshimiana na kulindwa maslahi ya pamoja.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 08, 2025 23:20 UTC
  • Iran: Tuko tayari kuimarisha uhusiano na Ulaya lakini kwa kuheshimiana

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesema kuwa, Tehran iko tayari kupanua uhusiano na nchi za Ulaya hususan Italia lakini kwa sharti la kuheshimiana na kulindwa maslahi ya pamoja.

Araghchi aliyasema hayo jana Jumapili alipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Riccardo Guariglia ambaye yupo hapa mjini Tehran kushiriki katika duru ya 5 ya mashauriano ya kisiasa baina ya Iran na Italia.

Amesema Iran na Italia zina uhusiano wa kiundani na wa kidugu katika nyanja tofauti za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameongeza kuwa, mashauriano ya mara kwa mara ya kisiasa kati ya Tehran na Roma yatakuwa na nafasi "muhimu na yenye ufanisi" katika kukuza uelewa mzuri wa misimamo na mitazamo ya pande zote mbili.

Amesisitiza kwa kusema: "Hii itazisaidia nchi hizi mbili kuimarisha uhusiano wa pande zote na kukuza utulivu na usalama katika ngazi ya kikanda na kimataifa".

Kwa upande wake mwanadiplomasia huyo wa Italia amesema kuwa amefurahi kuona kwamba ameweza kufanya mazungumzo chanya na viongozi wa Iran na kueleza nia ya nchi yake ya kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu Iran kwa kuzingatia maslahi ya pamoja.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na Masuala ya Kisiasa, Majid Takht-Ravanchi na Guariglia waliongoza duru ya tano ya mashauriano ya kisiasa ya Iran na Italia jana Jumapili hapa Tehran.

Katika kikao hicho pande hizo mbili zilijadili masuala mbali mbali yakiwemo mahusiano ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kibalozi pamoja na maendeleo ya kieneo na kimataifa yakiwemo mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani.