Duru ya sita ya mazungumzo ya Iran na Marekani kufanyika Jumapili ijayo
Duru ya sita ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya Iran na Marekani yanatajiwa kufanyika Jumapili ijayo huko Muscat Oman.
Hayo yameelezwa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ambaye amethibitisha kwamba, duru ya sita ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani imepangwa kufanyika Jumapili ijayo mjini Muscat Oman. Oman ni mpatanishi wa mazungumzo hayo.
Esmail Baghaei ameeleza kuwa, tayari maandalizi kwa ajili ya mazungumzo ya duru ya sita huko Oman yamekamilika.
Mazungumzo haya yanakuja wakati ambapo Iran na Marekani zinajaribu kufikia makubaliano kuhusu masuala ya nyuklia. Matokeo ya majadiliano yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mustakabali wa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kidiplomasia kupunguza mivutano na kutafuta muafaka. Muscat, kama mwenyeji, ina jukumu muhimu katika upatanishi kati ya Iran na Marekani.
Iran na Marekani tayari zimefanya duru tano za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ili kutafuta njia mbadala ya Mkataba wa Nyuklia wa 2015 (maarufu kama JCPOA).
Hata hivyo, mazungumzo hayo yamekwama kutokana na shinikizo la Marekani kwamba Iran iache kabisa utajirishaji wa urani chini ya mkataba wowote mpya, sharti ambalo Tehran imelipinga vikali.
Maafisa wa Iran wameweka wazi kuwa hawatakubali kupokonywa haki yao ya msingi katika sekta ya nyuklia, wakisisitiza kuwa shughuli zao hazilengi utengenezaji wa silaha za nyuklia, bali ni kwa matumizi ya kiraia na maendeleo ya kitaifa.