Iran: Operesheni yetu ya kiintelijensia imeyumbisha vikali usalama wa Israel
Wizara ya Usalama wa Taifa (Intelijensia) ya Iran imetoa taarifa kuhusu mafanikio yake makubwa ya kukusanya na kuhamisha nyaraka nyingi za siri kutoka Israel, na kuieleza operesheni hiyo kama ushindi wa kipekee na wa kihistoria wa kijasusi ambao haujawahi kushuhudiwa.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa Jumanne, wizara hiyo imesema mafanikio hayo yameupa pigo kubwa “utawala wa Kizayuni” na kutikisa taswira yake ya kutopenyeka, huku ikikitaja kilichofanyika kama “tukio la kihistoria” katika historia ya kushindwa kiusalama utawala huo. Wizara hiyo pia imesema ushindi huo ni wa kihistoria na ni alama ya mafanikio kwa "Mhimili wa Muqawama".
Taarifa hiyo imesema kuwa nyaraka hizo zimepatikana wakati ambapo Israel imekuwa ikijitahidi kuonesha kuwa hakuna adui anayeweza kujipenyeza na kupata taarifa zake za siri. Israel haikutarajia mapungufu katika mfumo wake wa kiusalama.
Hali kadhalika taarifa hiyo imebaini kuwa: “Wakati walikuwa bado wakijadili makosa ya kiintelijensia ya huko nyuma na wakiamini kuwa wamefunga kila njia ya upenyezaji, walikumbwa na operesheni ya kihistoria ya ‘Kimbunga cha Al-Aqsa’ iliyotekelezwa na wapiganaji shujaa wa Kipalestina, na kuanika kwa uwazi kasoro kubwa ya kiusalama na kijasusi.”
Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imefafanua kuwa operesheni hiyo ilitekelezwa pamoja na kuwepo ulinzi mkali uliowekwa na Israel, na kwamba mbinu zilizotumiwa kufikia na kuondoa nyaraka hizo kutoka maeneo yanayokaliwa kimabavu (Israel) zilikuwa za hali ya juu kiasi kwamba zilishinda mifumo yote ya ulinzi ya Israel.
Taarifa hiyo aidha imesema: “Utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa umeweka protokali kali kabisa kwa ajili ya kulinda nyaraka hizo za kimkakati. Kwa msingi huo maajenti wetu walilazimika kutumia mpango wa kina na wa hali ya juu, ambao hadi sasa haujafahamika wala kueleweka kwa mfumo wowote wa usalama wa Israel.”
Wizara hiyo imeongeza kuwa sehemu kubwa ya nyaraka hizo tayari inatumiwa na vikosi vya kijeshi nchini Iran, huku sehemu nyingine zikiwa tayari kutolewa kwa nchi rafiki au kwa makundi yanayopinga utawala wa Kizayuni.
Taarifa hiyo pia imesema kuwa nyaraka hizo zinaonesha kiwango cha juu cha msaada wa mataifa ya Magharibi kwa mpango wa silaha za nyuklia wa Israel, jambo ambalo wizara imelaani na kulitaja kuwa ni "unafiki mkubwa", kwa kuzingatia kuwa nchi hizo hizo zimekuwa zikiishinikiza Iran kwa miongo kadhaa kwa madai ya kutengeneza silaha za nyuklia.
Miongoni mwa mambo yaliyoanikwa na nyaraka hizo ni ripoti nyingi za uzushi ambazo Israel ilipeleka kwa mashirika ya kimataifa, ikidai kuwa mpango wa nyuklia wa Iran si wa amani. Taarifa hiyo imeeleza kuwa mashirika hayo yalinukuu tuhuma hizo bila utafiti wa kina.
Iran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani na wa maendeleo ya kisayansi ya taifa hili huku ikikanusha kwa muda mrefu madai ya Magharibi kwamba inalenga kutengeneza silaha za nyuklia.