Iran yataka kikao cha Baraza la Usalama, UN yakubali
(last modified Fri, 13 Jun 2025 13:31:57 GMT )
Jun 13, 2025 13:31 UTC
  • Iran yataka kikao cha Baraza la Usalama, UN yakubali

Katika barua ya dharura kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa huko New York Marekani ametoa mwito wa kufanyika kikao cha dharura cha kulaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya vituo vya nyuklia na mauaji ya maafisa wa kijeshi wa Iran. Kwa upande wake, Umoja wa Mataifa umekubali kuitisha kikao hicho cha dharura.

Katika barua rasmi na ya dharura iliyotumwa kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa "Amir Saeed Iravani," Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa sambamba na kulaani vikali mashambulizi ya utawala wa Kizayuni kwa msaada kamili wa Marekani dhidi ya vituo vya amani vya nyuklia na maafisa wakuu wa kijeshi wa Iran, ametoa mwito wa kuitishwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama na kuchukuliwa hatua za dharura za kujibu jinai hizo za Israel.

Barua hiyo imesisitiza kuwa: "Utawala wa Kizayuni umefanya mashambulizi yaliyoratibiwa zamani dhidi ya vituo vya nyuklia na miundombinu ya kiraia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hatua hizo ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na misingi mikuu ya sheria za kimataifa, na matokeo yake ni ya hatari na yanatishia mno amani na usalama wa kieneo na kimataifa."

Wakati huo huo duru moja ya kuaminika imekanusha uvumi kwamba Jamhuri ya Kiislamu imepeleka droni za kulipigiza kisasi na amesema: Iran bado haijafanya shambulio lolote la ndege zisizo na rubani. Duru hiyo imeliambia shirika la habari la Fars kuhusu uvumi huo kwamba: Habari hiyo haijathibitishwa, kisasi cha kweli kitafanyika katika siku za usoni na kitaripotiwa tu kupitia vyanzo rasmi.

Asubuhi ya leo Ijumaa, baadhi ya vyombo vya habari vya Kizayuni vimeeneza uvumi kwamba Iran imejibu mashambulizi ya Israel kwa kutuma makumi ya ndege zisizo na rubani lakini ndege zote hizo zimetunguliwa. Kwa mara nyingine amesema, wakati Iran itakapotoa majibu yake, yataripotiwa kupitia duru rasmi.