Iran yaapa kulipiza kisasi baada ya Australia kumfukuza balozi wake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130022-iran_yaapa_kulipiza_kisasi_baada_ya_australia_kumfukuza_balozi_wake
Iran imeapa kuchukua hatua zinazofaa za kulipiza kisasi baada ya Australia kumfukuza balozi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini humo kwa madai ya "chuki dhidi ya Wayahudi," na kusisitiza kwamba vitendo vya ubaguzi wa kidini havina nafasi katika utamaduni, historia au imani ya taifa la Iran.
(last modified 2025-08-26T15:13:46+00:00 )
Aug 26, 2025 15:13 UTC
  • Iran yaapa kulipiza kisasi baada ya Australia kumfukuza balozi wake

Iran imeapa kuchukua hatua zinazofaa za kulipiza kisasi baada ya Australia kumfukuza balozi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini humo kwa madai ya "chuki dhidi ya Wayahudi," na kusisitiza kwamba vitendo vya ubaguzi wa kidini havina nafasi katika utamaduni, historia au imani ya taifa la Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amesema hayo kwenye mkutano wa waandishi wa habari leo Jumanne mjini Tehran, muda mfupi baada ya Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese kutangaza habari ya kufukuzwa balozi wa Iran nchini humo kwa madai ya chuki dhidi ya Mayahudi bila kutoa ushahidi wowote.

Baqaei amesema, Iran inapinga shutuma kama hizo kwa nguvu zote, na kuahidi kulipiza kisasi dhidi ya hatua yoyote kama hiyo ya "kidiplomasia isiyofaa na isiyo na uhalali".

Akipuuzilia mbali kuwepo kwa mielekeo yoyote ya chuki dhidi ya Wayahudi katika historia ya utamaduni na ya kidini ya Iran, msemaji Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, "Jambo hili ni sifa ya nchi za Magharibi na Ulaya."

“Ukiangalia historia, kuteswa kwa Mayahudi kwa sababu ya dini yao ni suala ambalo limekita mizizi huko Ulaya, na ni wao ambao wanapaswa kuwajibika kwa historia yao ya zamani, ambayo imeendelea hadi leo."

Baqaie ameongeza kuwa, uamuzi wa Canberra ni jaribio la kuhalalisha sera zake dhidi ya Iran na kufidia matukio machache na adimu ya ukosoaji dhidi ya Israel ambayo yameshuhudiwa hivi karibuni kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wa Australia, akiwemo Waalbanese mwenyewe.