Iran yaitaka dunia ilaani mashambulizi dhidi ya vituo vyake vya nyuklia
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Iran amesema Marekani na utawala wa Israel zilifanya mashambulizi ya kimakusudi dhidi ya vituo vya nyuklia ya Iran, licha ya vituo hivyo kuwa chini ya usimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Nyuklia.
Amir-Saeid Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameyasema hayo na kuongeza kuwa, "Mashambulizi hayo yalilenga kabisa kitovu cha NPT (Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia)."
Alisema hayo katika hotuba aliyoitoa kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Majaribio ya Nyuklia na kubainisha kuwa, "Ningependa kuungana na wajumbe wengine kuipongeza Kazakhstan kwa hatua yake ya kutangaza Siku ya Kimataifa Dhidi ya Majaribio ya Nyuklia."
Iravani amesema, Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Majaribio ya Nyuklia ilianzishwa ili kukumbusha ulimwengu juu ya matokeo mabaya ya majaribio ya nyuklia kwa afya ya binadamu, mazingira, amani na usalama wa kimataifa, matokeo ambayo yanaacha alama ya kudumu kwa wanadamu na mazingira kwa vizazi vijavyo.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa: Hatari zinazoletwa na majaribio ya nyuklia haziishii kwenye ulipuaji wa makusudi pekee; bali kushambuliwa kwa makusudi suhula za nyuklia ni hatari kwa usalama wa dunia. Mashambulizi ya hivi karibuni ya kizembe ya utawala wa Israel na Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran yanadhihirisha wasiwasi huu wa dharura.
Hivi karibuni pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi alisema kuwa, "Mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya vituo vyetu vya nyuklia yalikiuka wazi NPT na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo liliidhinisha makubaliano ua nyuklia ya Iran mwaka 2015."
Mnamo Juni 13, Israel ilianzisha uchokozi wa wazi na usio na msingi dhidi ya Iran, na kuwaua makamanda kadhaa wa ngazi za juu wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia wa nchi hii. Tarehe 22 Juni, Marekani ilijiunga rasmi na vita hivyo vya kichokozi vya Israel dhidi ya Iran, kwa kutekeleza mashambulizi kwenye vituo vitatu vya nyuklia hapa nchini, kinyume na NPT.