Rais wa Iran kuhudhuria kikao cha nchi za Kiislamu na Kiarabu cha Doha kujadili uchokozi wa Israel
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran atahudhuria kikao cha dharura cha nchi za Kiislamu na Kiarabu kitakachofanyika mjini Doha siku ya Jumapili na Jumatatu kwa wito wa serikali ya Qatar, ili kuwaunga mkono Wapalestina wa Ghaza na kuchukua hatua dhidi ya shambulio la hivi karibuni lililofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel katika mji mkuu wa Qatar, Doha.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi amethibitisha ushiriki wa Iran, na kueleza kwamba yeye na Rais Pezeshkian watahutubia kikao hicho.
Akizungumza katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, IRIB, Araghchi amesema: "ni wakati wa kuchukua hatua za kivitendo, maneno pekee hayatoshi," na akasisitiza kwamba mkutano huo lazima uende mbali zaidi ya kutosheka na kauli za kulaani tu.
Kikao cha Doha kitafanyika baada ya utawala ghasibu wa Israel kufanya shambulizi la makombora katika mji mkuu huo wa Qatar siku ya Jumanne iliyopita, lililowalenga viongozi wakuu wa harakati ya ukombozi wa Palestina ya Hamas. Shambulio hilo, ambalo liliua jamaa na wasaidizi wa maafisa wa Hamas na kutofaulu kuwaua viongozi waandamizi wa harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, limelaaniwa vikali likiwa ni shambulio la kwanza la kufanywa na Israel ndani ya ardhi ya Qatar. Qatar imesisitiza kutolewa mjibizo wa pamoja wa kikanda dhidi ya jinai hiyo ya utawala wa kizayuni.
Katika mahojiano hayo na IRIB, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekumbusha kuwa katika kikao cha mwisho cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC kilichofanyika mjini Jeddah, Saudi Arabia, Tehran ilisisitiza juu ya kuchukuliwa hatua madhubuti dhidi ya utawala haramu wa Israel.
"Tulipendekeza kuvunjwa uhusiano na utawala wa Kizayuni, kukomeshwa ushirikiano wa kiuchumi, kutishia wale walio upande wa Israel na Magharibi, na kuweka vikwazo na adhabu za kiuchumi," ameeleza Araghchi na kuongeza kuwa kungali kuna umuhimu wa kuchukuliwa hatua kama hizo.
Wakati huohuo, serikali ya Qatar imetangaza kuwa, mbali na kikao cha dharura cha Doha na hatua za pamoja zitakazochukuliwa, imezungumza pia na timu yake ya wanasheria juu ya namna ya kumuwajibisha Waziri mkuu wa utawala wa kizayuni Benjamin Netanyahu kwa kuhusika na uvunjaji wa sheria za kimataifa.../