Jenerali: Uwezo wa Iran wa kivita unawazuia maadui kuanzisha mashambulizi mapya
Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi, amepongeza kuimarika kwa uwezo wa kujihami wa taifa , akisisitiza kuwa utayari wa Iran wa kivita umezuia maadui kuanzisha duru mpya ya mashambulizi dhidi ya nchi.
Akizungumza Jumatano, alipokuwa akizuru makao makuu ya Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) mjini Tehran, Mousavi alisema: “Uwezo wetu wa kujihami na utayari wa kivita umefikia kiwango kinachozuia maadui kufanya makosa ya kimkakati, ikiwemo wazo la kuivamia tena nchi yetu.”
Kiongozi huyo wa kijeshi wa ngazi ya juu alisifu utayari wa kina wa vikosi vya Iran katika kulinda uhuru wa taifa, usalama wa ndani, na mipaka ya ardhi, sambamba na kukabiliana na vitisho vyote vinavyoweza kujitokeza.
Mousavi pia alitambua umakini na busara ya vikosi vya ulinzi, akavipongeza kwa tajriba yao ya kihistoria, hususan katika vita vya mwaka 1980 hadi 1988 vilivyolazimishwa na dikteta wa Iraq wa wakati huo, Saddam Hussein, pamoja na operesheni ya siku 12 ya kijeshi iliyozinduliwa na Israel na Marekani mnamo mwezi Juni.
Jenerali huyo alieleza kuwa kuongezeka kwa uwezo wa kijeshi na wa kujihami katika nyanja mbalimbali ni mkakati usioepukika, akisisitiza kuwa hatua hizo zinaleta usalama endelevu na kuimarisha uwezo wa Iran wa kuzuia mashambulizi ya aina yoyote dhidi ya taifa hilo.
Mnamo Juni 13, utawala wa Israel ulianzisha mashambulizi haramu dhidi ya Iran, na kusababisha mauaji ya makamanda waandamizi, wanasayansi wa nyuklia, na raia wa kawaida.
Iran ilijibu ndani ya saa 24 kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani katika operesheni ya kulipiza kisasi iliyoendelea kwa siku 12. Marekani iliingia vitani kwa niaba ya Israel mnamo Juni 22, ambapo ndege zake za kivita zilishambulia vituo vitatu vya nyuklia vya Iran, kwa ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Kama jibu, Iran ilirusha makombora dhidi ya Kituo cha Kijeshi cha Anga cha Al Udeid kilichoko Qatar—kituo kikubwa zaidi cha kijeshi cha Marekani katika Asia ya Magharibi—kama hatua ya kujilinda.
Hatimaye, utawala wa Israel, ambao tayari ulikuwa umepata kipigo kikali kutoka Iran, ulilazimika kuomba mapatano ya kusitisha mapigano bila masharti mnamo Juni 24.