Saudia yaitaarifu rasmi Iran makubaliano yake ya kijeshi na Pakistan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amefanya mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran n kumtaarifu rasmi kuhusu makubaliano ya hivi karibuni ya ulinzi ya Saudia na Pakistan.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Abbas Araqchi alifahamishwa hayo jana Alkhamisi, Septemba 18, 2025 na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi, Faisal bin Farhan.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zimejadiliana pia namna ya kutia nguvu uhusiano baina yao na matukio ya kikanda na kimataifa.
Saudi Arabia na Pakistan zilitia saini makubaliano ya ulinzi wa kimkakati juzi Jumatano, na kukubaliana kwamba uchokozi wowote dhidi ya moja ya nchi hizo mbili ni sawa na uchokozi dhidi ya nchi zote mbili.
Shirika rasmi la wanahabari la Saudia liliripoti Jumatano jioni kwamba makubaliano hayo yalitiwa saini wakati wa mkutano rasmi kati ya Mwanamfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman na Waziri Mkuu wa Pakistan, Muhammad Shehbaz Sharif katika Kasri ya Al Yamamah mjini Riyadh. Shirika la habari la Reuters pia limetaja makubaliano hayo kuwa ni ishara ya kuimarika ushirikiano wa kiusalama uliodumu kwa miongo kadhaa kati ya nchi hizo mbili. Ofisi ya Waziri Mkuu wa Pakistan pia imesema lengo la makubaliano hayo ni kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi kati ya nchi hizo mbili na kuzuia uchokozi wa aina yoyote dhidi ya pande hizo.
Makubaliano haya yamekuja baada ya Israel kushambulia kigaidi Doha, mji mkuu wa Qatar, Jumanne ya wiki iliyopita.