Iran yaibuka ya 3 katika Mashindano ya Riadha ya Walemavu India
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i131696-iran_yaibuka_ya_3_katika_mashindano_ya_riadha_ya_walemavu_india
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemaliza katika nafasi ya tatu katika Duru ya 12 ya Mashindano ya Riadha ya Walemavu yaliyofanyika nchini India.
(last modified 2025-10-07T02:38:47+00:00 )
Oct 07, 2025 02:38 UTC
  • Iran yaibuka ya 3 katika Mashindano ya Riadha ya Walemavu India

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemaliza katika nafasi ya tatu katika Duru ya 12 ya Mashindano ya Riadha ya Walemavu yaliyofanyika nchini India.

Wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameng'ara kwenye mashindano hayo ya kimataifa kwa kujinyakulia medali tisa za dhahabu, mbili za fedha na tano za shaba katika michezo tofauti ikiwemo kurush tufe, kisahani, na mshale.

Baada ya wanariadha wa Iran kuibuka wa tatu katika Mashindano ya Riadha ya Dunia ya 2025, Aliasghar Hadizadeh, Mkuu wa Chama cha Wanariadha wa Iran, amesifu na kupongeza umbuji wa wanamichezo hao wa Iran, kwa kupeperusha juu bendera ya Jamhuri ya Kiislamu.

"Mchezo wa wanariadha wetu ulionyesha mafanikio ya kihistoria kwenye mashindano hayo. Hapo awali hatukuwa tumefikia kiwango kama hicho. Matokeo yetu bora zaidi ya awali yalikuwa ni medali nne za dhahabu katika kampeni moja, na huko Paris, Kobe, Dubai, na London, tuliweza kupata dhahabu tatu pekee," Hadizadeh ameliambia gazeti la Tehran Times.

Ameeleza kuwa, "Natumai wanariadha wetu wanaweza kuendeleza kasi hii na kufanya vyema katika Michezo ya Asia ya 2026 huko Nagoya na Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya 2028 huko Los Angeles. Ninawashukuru wanariadha wote, makocha, na mashabiki ambao walisimama pamoja na timu yetu huko Delhi na kuitakia ushindi endelevu," ameongeza.

Mashindano hayo ya kimataifa yalianza Septemba 26 hadi Oktoba 5 katika Uwanja wa Jawaharlal Nehru huko New Delhi, India. Brazil iliongoza jedwali la medali kwa kuzoa medali 44 (15 za dhahabu, 20 za fedha, 9 za shaba). China iliambulia dhahabu 13, fedha 22, na shaba 17 (jumla ya medali 52) lakini ilimaliza ya pili kutokana na kuwa na dhahabu mbili pungufu, nyuma ya Brazil.

Wakati huo huo, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa, uanamichezo na kuakisi utamaduni wa Kiislamu wa Iran kutazipa thamani kubwa medali za wanariadha wa nchi hii katika duru ijayo ya Michezo ya Mshikamano wa Kiislamu mjini Riyadh.

Katika ujumbe wake wa jana Jumatatu kwa timu ya michezo wa Iran kabla ya mashindano hayo, Pezeshkian amewatakia mafanikio wanariadha hao na kuwataka kuliwakilisha taifa kwa heshima. "Mnastahili kushinda medali za kupendeza katika Michezo ya Vijana ya Asia nchini Bahrain na Michezo ya Mshikamano wa Kiislamu huko Riyadh," amesema. "Lakini kinachofanya medali zako kuwa za thamani zaidi ni uchezaji na udhihirisho wa utamaduni wa Irani na Uislamu katika mashindano."