Russia yasisitizia mazungumzo chanya baina yake na Iran na Uturuki kuhusu Syria
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema, mazungumzo ya pande tatu yanayoendelea baina ya nchi hiyo na Iran na Uturuki kuhusu Syria ni yenye taathira chanya.
Maria Zakharova ameyaeleza hayo mbele ya waandishi wa habari mjini Moscow na kubainisha kuwa mazungumzo baina ya Russia, Iran na Uturuki kuhusiana na kutatua mgogoro wa Syria na eneo ni " ya ufanisi na yenye taathira".
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameashiria pia mazungumzo ya nchi yake na Marekani na kueleza kuwa harakati za pamoja za Moscow na Washington kuhusiana na Syria zimefikia kwenye awamu muhimu sana.
Kuhusiana na hitilafu za mitazamo zilizopo baina ya Russia na Uturuki juu ya kadhia ya Syria, Zakharov amesema hitilafu haziwezi kutatuliwa kwa siku moja lakini mawasiliano yanayoendelea kufanyika hivi sasa ni ya kutia matumaini.
Baada ya safari ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif nchini Uturuki, duru mbalimbali za habari zimedokeza kuhusu kuanzishwa ushirikiano wa pande tatu baina ya Iran, Uturuki na Russia kwa lengo la kutatua mgogoro wa Syria na kurejesha uthabiti nchini humo.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa imechangiwa na kubadilika msimamo na muelekeo wa serikali ya Uturuki kuhusiana na madola ya Magharibi kufuatia jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililotokea hivi karibuni nchini humo.../