Iran yasema haitashiriki Kombe la Dunia la FIFA 2026
Waziri wa Michezo wa Iran, Ahmad Donyamali amesema timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu haitashiriki katika fainali za Kombe la Dunia katika msimu ujao wa joto, licha ya Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, Gianni Infantino kusisitiza kuwa amehakikishiwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwamba Iran inakaribishwa kushiriki mashindano hayo makubwa zaidi ya soka duniani, pamoja na vita vinavyoendelea.
Donyamali ameiambia televisheni ya taifa kuwa, "Kwa kuzingatia kuwa utawala huu fisadi umemuua kigaidi Kiongozi wetu (Ayatullah Ali Khamenei), kwa namna yoyote ile hatuwezi kushiriki katika Kombe la Dunia."
Iran imepangwa katika Kundi G pamoja na Misri, New Zealand na Ubelgiji, ambapo mechi za pote hilo zimeratibiwa kupigwa nchini Marekani. Marekani inatazamiwa kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la FIFA msimu wa joto mwaka huu, ikishirikiana na Canada na Mexico.
Waziri wa Michezo wa Iran ameeleza bayana kuwa: Watoto wetu hawapo salama, na kimsingi, hayo mazingira hayaruhusu washiriki (katika Kombe la Dunia).
Donyamali amebainisha kuwa, "Kwa kutilia maanani vitendo viovu vilivyofanywa dhidi ya Iran, wametutwisha vita viwili ndani ya miezi minane au tisa, na wameua shahidi maelfu ya watu wetu. Kwa msingi huo, (timu ya soka ya Iran) haiwezi kushiriki (Kombe la Dunia).
Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari, Sepp Blatter, Rais wa zamani wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) aliwataka watazamaji wa Kombe la Dunia wasisafiri kwenda Marekani kutokana na wasiwasi wa kiusalama.
Aidha Rais wa Shirikisho la soka la Ujerumani (DFB) alisema hivi karibuni kuwa, ni wakati wakati wa kujiondoa kwenye Kombe la Dunia la 2026 kutokana na hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump. Mapema mwezi huo, Trump aliwakasirisha viongozi wa Ulaya kuhusu azma yake ya kutwaa kisiwa cha Greenland, ambacho sasa kinasimamiwa na Denmark.